Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewashukuru na kuwapongeza
madaktari wa Taasisi ya Bilal Muslim Tanzania iliyotoa huduma ya matibabu ya
macho kwa zaidi ya wananchi 4,000 wa mkoa wa Dodoma.
Ametoa pongezi hizo juzi wakati akizungumza na madaktari
waliotoa huduma hiyo walipomtembelea katika makazi yake mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema huduma wanayoitoa ni muhimu
kwa kuwa imewezesha watu ambao walikata tamaa ya kuona wameona, hivyo aliwaomba
waendelee kwenda katika maeneo mengine nchini ili Watanzania wengi zaidi waweze
kunufaika.
"Nawashukuru kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika
kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya macho
bure na kuwawezesha hata wale wasiokuwa na uwezo kupata huduma," alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati
kuwatumikia wananchi na kutoa huduma kwa wote, hivyo iko tayari kushirikiana na taasisi yeyote ambayo inakusudia
kuwafikia wananchi.
Alisema: “Katika utoaji huduma za jamii, Serikali
inathamini sana mchango wa taasisi binafsi na za dini ambazo ziko mstari wa
mbele kushirikiana na jamii kwa ujumla.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwakaribisha
madaktari hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani Dodoma.
“Hapa ndiyo makao makuu ya Tanzania, hivyo nawakaribisha
mje kuwekeza, ardhi ya kutosha ipo . Mnaweza kuja kujenga hospitali kubwa ya
macho," alisema.
Akizungumza katika tukio hilo, Naibu wa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira,
Anthony Mavunde alisema jumla ya watoto 250 wamefanyiwa upasuaji wa macho
na madaktari hao walioanza kutoa huduma hiyo Desemba 8, 2016 na kumaliza jana.
"Nawashukuru kwa moyo wenu wa kujitolea kuja
kusaidia watu wenye mahitaji ya matibabu ya macho. Mkoa wa Dodoma una changamoto
kubwa ya matatizo ya macho. Nimefarijika sana kuona baadhi ya kinamama waliokuwa wamekata
tamaa ya kuona wameweza kuona tena,” alisema.
Mratibu wa taasisi hiyo, Noorelain Sharrif alimuahidi
Waziri Mkuu kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma
za matibabu ya macho bure kwa wananchi wenye mahitaji na wako tayari kwenda
popote nchini kutoa huduma hiyo.
“Tuko tayari kushirikiana na Serikali katika kutimiza
wajibu wetu kwa jamii. Tutafanya hivyo wakati wowote na kwa wananchi wote,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment