Mwandishi Wetu, Mara
Profesa Makame Mbarawa |
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewapa miezi minne wakandarasi wazawa wa
Kampuni ya Ujenzi ya Daraja la Mbutu JV inayojenga barabara ya Makutano hadi Nata
wilayani Serengeti mkoani Mara kukamilisha kilomita 18 kati ya 50 za barabara
hiyo kwa kiwango cha lami.
Mbarawa alitoa agizo hilo, alipokuwa
akikagua mradi huo wa barabara inayoanzia makutano kupitia Butiama, Nyamuswa
hadi Sanzate ambao upo katika mkoa wa Mara na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi
wake ambayo imesuasua kwa takriban miaka mitatu sasa.
"Nataka mwezi Aprili mwakani sehemu
ya barabara hii iwe imeshakamilika kwa kiwango cha lami na wananchi waanze
kufurahia matunda yake. Hatuwezi kusubiri kwa muda wote huo kuwavumilia
kukamilisha mradi huu”, alisema.
Alisisitiza kuwa nia ya Serikali ya
kuboresha barabara hiyo ni kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha makazi,
kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya barabara hiyo na kuhamasisha utalii
kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads),
mkoa wa Mara, mhandisi Japherson Nnko alisema kuwa barabara hiyo
itakapomalizika itakuwa na njia ya magari yenye upana wa mita 6.5, mabega ya
barabara ya mita 1.5 kila upande na Daraja kubwa la Kyarano lenye urefu wa mita
37.5.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema
itawapa kipaumbele makandarasi wazawa kuweza kushiriki katika mradi wa ujenzi
wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge), inayotarajiwa kuanza hivi karibuni
katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali imewataka makandarasi
hao kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa kwa kuomba zabuni za ujenzi huo na
kuziimarisha kampuni zao, ikiwemo kuwa na vifaa vilivyo bora ili kupambana na
soko la kibiashara na makandarasi wa nje.
Sambamba na hayo, waziri amekagua Uwanja
wa Ndege wa Musoma na kusema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inapanua na
kujenga kwa kiwango cha lami uwanja huo, hususani njia ya kuruka na kutua ndege
kutoka kilomita 1.6 ya sasa hadi kilomita 1.8 ili kuruhusu ndege kubwa zenye
uwezo wa kubeba abiria 70 kutua.
0 comments:
Post a Comment