Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi
aliyekuwa Mhazini wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Issai Mbilu ambaye amehamishiwa
wilayani Bahi, Dodoma, na kuagiza arudishwe haraka kujibu tuhuma za ubadhirifu wa
Sh milioni 642.4 za miradi.
“Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu serikalini.
Ukiharibu Longido usitarajie kuhamishiwa wilaya nyingine, tunamalizana hapa
hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine, hivyo Mhazini
huyu arudishwe haraka Longido,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Longido, kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa kwenye ziara ya
kikazi mkoani Arusha.
Pia alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard
Kwitega kumwandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), amrudishe Mhazini huyo kwenye kituo chake cha
kazi cha zamani, ili ajibu tuhuma zake.
AlisemaSerikali haitavumilia mtumishi wa idara
yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishiwa sehemu nyingine. “Naagiza kuanzia
sasa nimemsimamisha kazi Mweka Hazina huyu na arudi hapa kujibu kwa nini
ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu.”
Majaliwa alisema miradi mingi ya maendeleo imekwama
kwa sababu baadhi ya watumishi huweka mbele maslahi binafsi, badala ya
kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo aliwaagiza wakuu wa idara wafuatilie kwa
makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, kama inalingana na thamani
halisi ya fedha zilizotolewa.
Akizungumzia kukithiri biashara haramu ya dawa za
kulevya Longido, Waziri Mkuu aliwaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Wilaya, kufanya msako wa nyumba kwa nyumba na kukamata watakaokutwa wakifanya
biashara hiyo.
“Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha dawa
za kulevya; bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua.
Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali
iko mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda, ili yawe na
ubora na thamani kubwa.
Alitoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi
katika kijiji cha Loonolwo, wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro.
Awali, wananchi hao waliokuwa na mabango,
walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya Longido na Ngorongoro,
ambapo Waziri Mkuu alimwagiza Ofisa Ardhi wa Mkoa wa Arusha, Hamdoun Mansour
kwenda vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza
mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment