Joyce Kasiki, Dodoma
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa
majambazi, wameuawa na wananchi waliovunja sheria kwa madai ya hasira, baada ya
wahusika kutuhumiwa kuteka na kupora fedha kwenye kituo cha mafuta cha Dabalo,
Chamwino mkoani hapa.
Akizungumza na waandisi wa habari
ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lazaro Mambosasa alisema mauaji
hayo yalifanyika Jumatano saa tatu usiku kijijini Dabalo.
Alidai kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi,
waliokuwa na pikipiki mbili moja namba T 194 CQF na nyingine aina ya SunLG isiyo
na namba, walipora Sh milioni 2.09.
Alisema baada ya kufanya unyang’anyi
huo, taarifa zilifika kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani ambao
walianza msako porini na kufunga barabara kijijini Segala.
“Majambazi walipofika kwenye kizuizi
hicho, waligeuza na kuelekea kijiji cha Manyemba ambako pia walikutana na kundi
la watu, wakafyatua risasi na kuwajeruhi Nyembela Mganga mguuni na mkewe
Ndalandala Nyembela, ambaye pia alijeruhiwa mguu; wote ni wakazi wa Manyemba,“ alisema
Kamanda Mambosasa.
Alifafanua kuwa wananchi hao
wakishirikiana na askari wawili wa kituo cha Polisi cha Dabalo, waliendelea na
msako na kuwakuta watuhumiwa hao porini, ambapo waliwashitukia wananchi na
kukimbilia Mlima Kinyami kijijini Hombolo, huku wakifyatua risasi angani kutishia
wananchi.
Mambosasa alisema licha ya majambazi hao
kufyatua risasi, wananchi hawakurudi nyuma ndipo nao wakakimbia pande tofauti
baada ya kuishiwa risasi.
Alisema wananchi waliendelea na hatimaye
kukamata watano na kati yao, watatu walishambuliwa na wananchi na kuwaua papo
hapo.
Aliwataja waliouawa kuwa ni Johnas
Mahanze ‘Chinaa’ mkazi wa Dakawa, Morogoro, Elias Kazembe wa Ifakara, Morogoro
na mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la utani la Mzungu mkazi wa Kiteto,
Manyara.
Alisema watuhumiwa waliokamatwa wakiwa
hai ni Shaban Sefu wa Dumila na Mashaka John wa kijiji cha Kikombo-Dabalo, Chamwino
na ndiye alikuwa mwenyeji wao.
Kamanda alisema watuhumiwa hao
walikamatwa na bunduki tatu aina ya shotgun; moja iliyofutwa namba, magobori
mawili na Sh 220,000 zilizokuwa sehemu ya mgao wa fedha walizopora.
0 comments:
Post a Comment