Jemah Makamba
KESI ya shambulizi na kudhuru mwili
inayomkabili Salum Njwete 'Scorpion', imeanza kusikilizwa kwa mlalamikaji, Said
Mrisho kutoa ushahidi jana.
Katika hali iliyoonesha simanzi, Mrisho
jana alifika kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala akisindikizwa na umati wa watu,
kisha kutoa ushahidi akiwa anabubujikwa machozi.
Aliiambia Mahakama kuwa anamtambua
aliyemfanyia ukatili huo kwa sura, kwani alimwona kabla ya kumtoboa macho.
Mrisho anakuwa shahidi wa kwanza kati ya
sita wanaotarajiwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo kwa upande wa mashitaka.
Mbele ya Hakimu Mkazi Frola Haule,
Mrisho alidai kuwa siku ya tukio alikuwa saluni Tabata na alifanya kazi siku
nzima hadi saa 8 usiku alipofunga na kwenda kituo cha daladala ambako akiwa
amesimama kituoni, alipita dereva wa bajaji na kumwambia aingie ili ampeleke
Buguruni.
"Nilimweleza dereva huyo siendi
Buguruni naenda Ubungo, hivyo akaniambia niingie akaniache Relini. Niliingia,
lakini tulipofika Barakuda, aliingia njia ya Buguruni ndipo nilipomuuliza mbona
unakwenda Buguruni na si Relini?"
Alisema dereva alimwomba amsaidie
akamshushe Buguruni, kwani bajaji yake haina mafuta ya kutosha kumfikisha
Ubungo. Alitaka akifika Buguruni apande gari la Ubungo.
Aliendelea kueleza kuwa alipofika
Buguruni aliona wafanyabiashara wa kuku wa kukaanga, aliosogea na kununua
akiomba auziwe kuku kwa Sh 6,000.
"Kabla sijachukua nilisikia mtu kwa
nyuma yangu akinigusa bega la kushoto, akisema ana shida anaomba nimsaidie.
Nilipomuuliza shida gani kama nitaweza nimsaidie hakujibu.
"Baadaye alifungua pochi aliyokuwa
amejifunga kiunoni na ghafla nilishangaa akinichoma visu vitatu mgongoni na
vinne tumboni."
Alidai kuwa muda wote huo alikuwa
akimwona vizuri kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa kutosha. Alidai kuwa alipiga
kelele kuomba msaada, lakini mtu huyo alisikika akitoa vitisho kuwa asisogee wa
kumsaidia.
Aliongeza kuwa baada ya hapo alimkanyaga
mkono na kumkatia kidani alichovaa mkononi na kumvua mkufu shingoni na kuchukua
pochi ikiwa na Sh 300,000.
Baada ya hapo alidai akiwa amelala chini
alisikia mtu akisema Scorpion ushaua huyo, ndipo mtuhumiwa akamshika mkono na
kumvutia barabarani na kumtupa katikati huku magari yakimkwepa, wakati
mshambuliaji akishinikiza madereva kumgonga.
"Baada ya kukwepwa nikiwa bado
naona, mtu huyo alinishika mkono na kunivutia pembeni na kunipekua mfukoni. Nilisikia sauti ya kijana muuza kuku
akisema kaka Salum mwachie simu zake, ushaua ili ndugu zake wapewe taarifa,
kauli ambayo ilimkera mtu huyo na
kumpiga teke kijana huyo.
"Alinichoma jicho la kushoto kwa
kisu na nilipoteza fahamu na nikaja kuzinduka baada ya muda na kusikia mtu
akisema yeye ni msamaria mwema anataka kunisaidia.
"Nilimtajia namba za mke wangu ili
ampigie simu na baada ya muda likaja gari ya Polisi na kunichukua hadi kituo
cha Polisi Buguruni ambako nilitoa maelezo kisha kupelekwa hospitali ya Amana
na baadaye Muhimbili."
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga,
alimhoji kama anaweza kumkumbuka mtuhumiwa alivyo na kitu gani anakumbuka
kutoka kwa aliyemfanyia tukio hilo.
Alijibu: "Nakumbuka, alikuwa mrefu,
maji ya kunde, ana mwili wa mazoezi na macho makubwa."
Hakimu alimwambia shahidi kuna maswali
ataulizwa na Wakili wa utetezi anayemtetea Njwete na anapaswa kuyajibu kama
anavyoulizwa.
Wakili wa mshitakiwa, Juma Nassoro
alimuuliza kwa nini kuna tofauti kubwa kati ya maelezo aliyotoa Polisi na
aliyotoa mbele ya Mahakama, alisema alikuwa haoni, hivyo hajui kilichoandikwa.
Alipoulizwa imekuaje asijue wakati
polisi husoma maelezo anayoyatoa mtu, alijibu: "Sikusomewa chochote na
polisi kwa hiyo sijui."
Alimuuliza kama ana taarifa kwamba yeye
ni mwizi na anahusika na matukio ya wizi Buguruni na alifika Buguruni kukununua
vitu vya wizi kama kawaida yake.
Mlalamikaji alisema si kweli yeye si
mwizi ambapo Wakili alimuuliza swali lingine la kama alishawahi kukamatwa kituo
cha Polisi chochote kwa tuhuma za wizi ambapo alikana.
Wakili alimuuliza sababu ya kituo cha
Polisi Buguruni kuwa vizuri katika utendaji kazi lakini tangu mwanzo wa tukio
hadi mwisho hakuna taarifa zilizofika na polisi kuja kumsaidia au kwa kuwa
walijua ni mwizi.
Shahidi alikana kuwa mwizi ambapo Wakili
wa utetezi alisema kuna raia watakuja kutoa ushahidi kuhusu matukio yake ya
wizi, shahidi akajibu sawa waje kutoa ushahidi.
Wakili wa Serikali alimuuliza swali moja
kwamba hata kama ni mwizi "je kuna mtu ana sheria ya kumtoboa mtu macho au
kumchoma kisu?" Akajibu "hapana".
Upande wa Jamhuri uliomba Hakimu
awapangie tarehe nyingine ya kuendelea na ushahidi, akaamua kesi hiyo itajwe
Desemba 28.
0 comments:
Post a Comment