Edith Msuya
Askofu William Mwamalang |
MWENYEKITI wa Kamati ya Taifa ya
Maaskofu na Mashekhe, Askofu William Mwamalanga, amemtaka Mchungaji wa Kanisa la
Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo kutoka hadharani na kuomba radhi waandishi wa
habari.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya
Mchungaji Lusekelo 'Mzee wa Upako', kusema kuwa waandishi wote walioandika
habari za kumchafua watakufa kabla ya Machi.
Akizungumza jana Dar es Salaam,
Mwamalanga alisema kauli hiyo si nzuri na imekosa maadili kwa kiongozi wa dini
kama yeye.
Alisema hakuna dini duniani inayoruhusu
kumtishia binadamu, kwani hata Mungu katika maandiko yake ya Korani au Biblia anaeleza
kuwa ni wa huruma na anahurumia watu wake.
Alisema ni vema Lusekelo akamrudia Mungu
wake kwa kutubu kwani hakuna mtu anayeweza kujilinganisha na Mungu.
"Alichokifanya Lusekelo ni kinyume
cha maadili, kwani hata Mungu anahurumia watu wake, hivyo ni vema akatoka
hadharani na kuomba radhi waandishi na Watanzania kwa jumla," alisema.
Aliongeza kuwa alichokifanya Mchungaji
huyo ni kosa la jinai, kwani si vema kutishia mtu maisha kwani hakuna binadamu
mwenye mamlaka hayo duniani.
"Kwa sababu walichoandika waandishi
wa habari alikifanya mwenyewe na hajasingiziwa kama anavyodai," alisema.
Mwamalanga alisema mbali na yote hayo,
Mchungaji huyo amemdhalilisha Rais John Magufuli kwani alimheshimu na kufika kwenye
Kanisa lake na kuzungumza naye na kumwonesha heshima ya juu.
0 comments:
Post a Comment