Celina Mathew
David Kafulila |
ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ameachana
na chama cha NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema, kwa alichoeleza kuwa ndicho chama
kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko mwaka 2020.
Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kujivua uanachama na kwamba anakwenda
Chadema.
Akizungumza na mwandishi wa JAMBO LEO jana, Kafulila
alisema hakufanya uamuzi huo kwa kukurupuka, bali kutokana na kutafakari na
kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, hivyo ameridhika na Chadema kwa kuwa ndiyo
sehemu inayojipambanua.
"Nimetafakari na kushauriwa sana jimboni na
nimeridhika, kwamba Chadema ndiyo sehemu iliyojipambanua kwa mikakati ya kuleta
mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya nguvu ya kila
mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha safari ya
mabadiliko," alisema.
"Leo (jana) nimewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa Chama
kumjulisha kwamba nimejivua uanachama na uongozi na nina mpango wa kurejea
Chadema," alifafanua Kafulila.
Alipotakiwa kufafanua kuhusu historia ya migogoro na
viongozi aliokuwa nao Chadema kabla ya kuhamia NCCR-Mageuzi, ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa alipata kumwita
‘sisimizi’ kwa alichoeleza kukosa imani naye, Kafulila alijibu kuwa siasa ni
malengo si uhusiano binafsi.
Aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa na malengo zaidi
ya urafiki na yeye malengo yake sasa ni kuendelea kupigania mabadiliko ya
kimfumo yanayoenea zaidi Chadema kuliko chama kingine.
Historia
Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua uanachama Chadema na
kuhamia NCCR –Mageuzi, baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Ofisa Habari aliyokuwanayo.
Akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa uanachama akidaiwa
kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka 'kumpindua' Mwenyekiti
James Mbatia.
Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu baada ya Mbatia
kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa mbunge, na wakiwa bungeni, Mbatia
na Kafulila walikutana, kuzungumza na kufikia uamuzi wa kumaliza mzozo
uliokuwapo.
0 comments:
Post a Comment