Celina Mathew
Ummy Mwalimu |
WAKATI ikielezwa kuwa ukatili wa
kijinsia unaigharimu Serikali asilimia saba ya pato ghafi la Taifa, yenyewe
imesema itaanzisha mtandao wa wanaume kila kata watakaokuwa na kazi ya kutetea
haki za wanawake na watoto wanaofanyiwa matukio hayo.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema
lengo ni kuhakikisha masuala ya ukatili ya kijinsia yanapungua kama si kukoma
kabisa.
Alisema pia wataanzisha madawati kwenye
shule za msingi na sekondari ili watoto wanaopata matatizo kama hayo wapate
msaada wa haraka.
"Kwa kweli tatizo la ukatili wa
kijinsia kwa wanawake na watoto ni changamoto kubwa na ni janga la dunia si
Tanzania tu, hivyo ni lazima tulidhibiti kwa kiasi kikubwa," alisema.
Alisema licha ya kuundwa kwa madawati kwenye
vituo vya Polisi pia wataanzisha kamati za ulinzi kila mtaa na kijiji, ili kuhakikisha
watoto na wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo, wahusika wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua.
0 comments:
Post a Comment