Waandishi Wetu
Rais Magufuli kanisani |
KAULI za kutaka Serikali, vyama vya siasa na wananchi kuombea amani
ya nchi ni mambo yaliyotawala katika mahubiri ya ibada za mkesha wa Krismasi
juzi na Krismasi yenyewe jana katika maeneo mbalimbali nchini.
Mbali na viongozi hao wa dini, Rais Magufuli akiwa katika Kanisa
Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Mjini Singida, alisisitiza suala la amani,
akisema ni muhimu kwa jamii yoyote inayopenda kupiga hatua katika maendeleo
yake.
Walichosema maaskofu Maaskofu, wachungaji na mapadri wa makanisa
mbalimbali walioendesha Ibada ya Krismasi walitumia muda mwingi kuhimiza amani,
huku baadhi yao wakisisitiza kuwa siku zote amani huletwa na maskini wasio na
kitu na sio matajiri.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo aliwataka watu kutambua kuwa amani ya kweli hailetwi na
matajiri au watu wenye utawala na mamlaka ya ulimwengu, bali huletwa na maskini
wasio na kitu.
Akitoa mafundisho katika mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la
Mtakatifu Joseph juzi usiku, Kadinali Pengo alisema masikini mwenye hamu ya
kupata utajiri ni hatari kuliko aliyerithi, iwapo atausaka utajiri huo kwa njia
zisizo halali.
“Amani hailetwi na matajiri wenye fedha, majumba mazuri…, kila
anayetaka amani anapaswa kutekeleza wajibu wake. Tukiomba amani tuwe wa kwanza
kutekeleza majukumu na wajibu wetu ili tuwe chimbuko kwa jirani na ndugu zetu.
Tunaodai amani tuwe wa kwanza kuwa mfano,” alisema.
“Si ufukara tu unaoweza kukuwezesha kuwa na amani, wapo masikini
wengi wanaotafuta mali kwa njia yoyote ile wakidhani watakuwa na amani kumbe si
kweli.
Haijalishi ni fukara kiasi gani kila mtu ana uwezo wa kuwa
chimbuko la amani miongoni mwa watu, unapotafuta usiseme mimi ni maskini, sina
uwezo wa kiutawala na kwamba huwezi kuwa na amani.”
Huku akisisitiza kuwa inaposakwa amani isitarajiwe kuwa italetwa
na wenye fedha, wanaostarehe, wanaokunywa kuzidi uwezo wao, alisema watu wa
kundi hilo wasitarajiwe kuwa ndiyo wasaka amani.
“Katika maisha ya sasa masikini ndio wanaokesha kulinda usalama wa
nchi zao na wao ndio watakaopewa kipaumbele katika habari ya ukombozi. Masikini
ndio wanaofanya kazi za matajiri kwa sababu hawajihusishi na anasa, hivyo matajiri
wanapokuwa wamelala kwa kushindwa kufanya kitu kutokana na kulewa wao
(masikini) hukesha wakifanya kazi,” alisema.
Alisema watu wengi hawaelewi sababu za Yesu Kristo kuzaliwa katika
hali ya umasikini na kusisitiza kuwa jambo hilo ni fumbo kubwa kwani licha ya
kuzaliwa katika familia hiyo, Yesu alihubiri neno la Mungu kwa masikini.
“Mungu anajiainisha kwa hao masikini na anaiainisha shughuli nzima
ya ukombozi kwa kuanza nao, dhiki ya ulimwengu siku ya leo ni kwa kila wenye
mapenzi mema maana mara nyingi tunadhani matajiri ndio wanaweza kuleta mali,”alisema
Kadinali Pengo.
Malasusa
atema cheche
Akizungumza katika Kanisa la Azania Front, Askofu wa Dayosisi ya
Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa aliitaka Serikali na vyama vya siasa kudumisha amani iliyodumu kwa
muda mrefu, kusisitiza “kamwe wasijaribu kuivunja.”
“Tunapaswa kuitunza bila kujali itikadi za kisiasa kwani ni zawadi
ya kipekee ambayo Mungu ametupatia. Yapo mataifa ambayo hadi leo yanahangaika
kuitafuta Amani ambayo sisi tunajivunia nayo, hii ni zawadi ambayo Mungu
aliamua kuipatia Tanzania hivyo tuitunze,” alisema.
“Niwaombe viongozi wetu na wanasiasa kuendeleza mshikamano kwani
ndio silaha kubwa ya ushindi.”
Katika ibada hiyo ambayo iliendeshwa na msaidizi wa Askofu huyo, Chidieli
Luiza ilienda sambamba na utoaji wa zawadi baina ya waumini kwa waumini, pia
Askofu Malasusa alitumia nafasi hiyo kutoa zawadi za kanisa kwa waumini.
Padri wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Alban, jijini Dar es
Salaam, Johnson Lameck alisema, “Tunapaswa kudumisha amani na upendo katika
mwaka ujao na tuhakikishe hatufanyi mambo yasiyofaa. Ujumbe wetu kama kanisa ni
‘amani’. Nchi yetu ni ya Amani tusiivuruge.”
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo alihubiri
amani kwa staili yake, pale alipoeleza kuwa baadhi ya vyombo vya habari
vinaandika habari za uongo na uzushi.
Lusekelo alisema tabia hiyo inachangia kuondoa amani katika jamii
na kama yeye angekuwa mtawala, angeminya uhuru wa habari. Katika ibada hiyo
Lusekelo ambaye hivi karibuni alisema waandishi wa habari walioandika habari za
kumchafua watakufa kabla ya Machi 2017 na baadaye kuwataka wamwombe radhi ili
awasamehe, alisema angekuwa mtawala angehakikisha anavibana vyombo vya habari
vinavyotoa habari za uchochezi.
Huku akitumia neno ‘uhuru wa kipumbavu’, alisema katika mitandao
ya kijamii watu wenye imani mbalimbali wamekuwa wakitumia lugha ya kibaguzi
jambo alilodai kuwa linatengeneza matabaka kwa waumini wa dini mbalimbali.
“Kuna watu wanalalamika makanisa yamekuwa mengi lakini wanashindwa
kulalamika kama baa zimekuwa nyingi mtaani, ukienda Sinza huwezi hata kupiga hatua
mbili utakuta baa,” alisema.
Alisema ikifika Juni mwakani waumini wa kanisa hilo watapata neema
na baraka ya aina yake, huku akiwashukia maadui zake kuwa mpaka kufikia kipindi
hicho watakuwa kimya.
Rais
Magufuli na amani
Rais Magufuli ambaye alishiriki ibada ya Krismasi jana katika
Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mjini Singida, aliwataka wananchi
kuendeleza amani na upendo na kuacha vitendo vya kubaguana kwa misingi ya dini,
kabila, itikadi na kanda zao.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa misa hiyo iliyoongozwa na
Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Edward Mapunda Rais Magufuli alisema, “Watanzania
wanatakiwa kuongeza juhudi katika kuchapa kazi kama alivyofanya Bwana Yesu.”
Alisema maeneo mengi nchini yanaonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua
na hivyo akawataka wananchi kutumia mvua chache zinazoendelea kunyesha
kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka upungufu wa chakula.
Rais aliwasisitiza wakazi wa mkoa wa Singida kunakolimwa alizeti
kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda ili kuzalisha mafuta ya kupikia kwa
wingi kwa kutumia zao hilo.
Imeandikwa
na Celina Mathew, Charles James, Mary Mtuka na Jemah Makamba
0 comments:
Post a Comment