Suleiman Msuya
SEKTA ya uvuvi nchini, imetajwa
kuchangia asilimia 2.4 ya pato la Taifa wakati ukuaji wake ukiwa wa kasi ya
asilimia 5.5.
Katibu Mkuu Wizara Mifugo, Kilimo na
Uvuvi, Sekta ya Uvuvi, Dk Yohana Budeba alisema hayo jana kwenye mahojiano
maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Alisema sekta ya uvuvi ni muhimu katika
uchumi wa nchi, hivyo inapaswa kupewa msukumo mkubwa.
Dk Budeba alisema kwa sasa sekta hiyo
inagusa kundi kubwa la jamii, hivyo mkakati ni kuona mchango wake kwa jamii na
nchi unaongezeka kwa kasi kubwa.
Alisema mwaka jana, tani 42,000 za
samaki ziliuzwa na kuiingizia Serikali Sh bilioni 7.5.
Dk Budeba alisema katika kuboresha sekta
hiyo na wavuvi kuvua kwenye maji marefu, samaki watapatikana kwa wingi kama
Serikali italipia asilimia 40 ya gharama za injini na vikundi vya wavuvi
kulipia asilimia 60.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku
ya chakula cha samaki kwa vikundi vya wavuvi, ili kuwaongeza nguvu na
kuwapunguzia gharama.
"Mwaka jana, ilitoa Sh milioni 440
zilizonunua boti za kuvulia na kugawiwa kwa vikundi vya wavuvi," alisema.
Alisema pia ada ya leseni ya uvuvi
imepunguzwa hadi Sh. 50,000 kwa mwaka na wavuvi wana uwezo wa kukata leseni ya
miezi mitatu au sita.
Aliwataka wavuvi kujiunga na vikundi ili
wapate elimu ya uvuvi wa kisasa, ruzuku na mikopo ya benki.
Katibu Mkuu huyo alisema Serikali
imeanzisha kikosikazi kinachojumuisha wizara tano ili kukabiliana na uvuvi
haramu, aliosema kuwa unatishia uwepo wa samaki na viwanda vidogo.
Dk Budeba alisema pamoja na changamoto
zilizopo, sekta ya uvuvi imetoa ajira ya kudumu kwa wavuvi 185,000.
Hali kadhalika Serikali imejenga
vitotoleshi vya samaki, ili kusaidia Watanzania kupata mbegu bora za samaki na
mwitikio wa ufugaji samaki wa kisasa ni mkubwa.
Katibu Mkuu alisema Serikali inatarajia
kujenga bandari ya uvuvi ili kuboresha sekta ya uvuvi nchini.
0 comments:
Post a Comment