Waandishi Wetu
WAKATI mwaka 2016 ukielekea ukingoni,
hotuba tano zilizotolewa na Rais John Magufuli zimetajwa kuwa ndizo
zilizotikisa zikitoa mwelekeo wa uongozi wake, Taifa na changamoto, huku
wachambuzi mbalimbali nchini wakizichambua na kueleza watarajio yao kwa mwaka
ujao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
JAMBO LEO, wachambuzi hao wamesema katika hotuba hizo ameweza kuonesha mweleko
mzuri katika masuala mbalimbali yaliyoonekana kutaka kuitikisa nchi yakiwemo; ubadhilifu,
uwajibikaji, rushwa, ufisadi, elimu, watumishi hewa na uchumi.
Tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Awamu ya
Tano Novemba 5 mwaka jana, Dk Magufuli amesafiri nje ya nchi mara mbili tu,
muda mwingi akiutumia ‘kuweka nchi sawa’, huku mara kadhaa akinukuliwa akisema mtangulizi
wake, Jakaya Kikwete amemwachia kazi ngumu kutokana na nchi kuwa ya wapiga dili
kila kona.
Hotuba hizo tano ni ile aliyoitoa wakati
wa uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ufunguzi wa
mkutano wa wahandisi, alipokabidhiwa uwenyekiti wa CCM, kuapishwa kwa makatibu
wakuu na naibu makatibu wakuu Ikulu na alipozungumza na wana CCM kwa mara ya
kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu.
“Amekuwa
muwazi katika vita dhidi ya kupambana na rushwa na
ufisadi. Wakati wa kampeni aliahidi kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kweli
ameanzisha, jambo ambalo limejenga imani kubwa kwa wananchi,” alisema George
Kahangwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu Dar es Salaam
(Udassa).
“Alisistiza kuhusu uwajibikaji na sasa
tunauona mafanikio. Hapo ndipo ulipoanza ule msemo wa ‘kutumbua majipu’ lengo
likiwa kuhakikisha wazembe wanakaa kando na wanaobaki wanafanya kazi ipasavyo
na kuachana na mazoea.”
Dk Kahangwa alisema kiongozi mkuu huyo
wa nchi pia amejitahidi kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, ikiwa ni
pamoja na kuvifufua vilivyokufa sambamba na kukaribisha wawekezaji huku akitea
mfano wa mvutano ulioibuka hivi karibuni kati ya Serikali na kiwanda cha saruji
cha Dangote.
Hamad Salim wa Chuo Kikuu Huria (OUT),
aliungana na Dk Kahangwa kuhusu mahakama ya mafisadi, kusisitiza kuwa ni jambo
ambalo halikutarajiwa kuwepo nchini.
“Yapo mambo ambayo ameweka njia ingawa
yanaweza kuwa na changamoto zake. Mfano ni elimu bure bado kuna changamoto
kadhaa sambamba na uanzishwaji wa viwanda,” alisema.
Alisema mkakati wa Serikali kuhakiki
vyeti vya watumishi wake umefungua njia ya kudhibiti mapato na matumizi
kutokana na kuwepo kwa kundi kubwa la wafanyakazi hewa waliokuwa wakikwamisha
kupatikana kwa fedha kwa ajili ya maendeleo.
“Ameweka msingi mzuri katika baadhi ya
mambo kama elimu bure, uwajibikaji na uchumi wa viwanda ingawa bado matunda
hayajaonekana. Nadhani anakwama kwa sababu ya kukosekana kwa sera maalum kwa
ajili ya kuzinyanyua sekta za viwanda, elimu na hata kupambana na mafisadi,”
alisema Profesa Gaudence Mpangala, Mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu Ruaha.
Wakati Profesa Mpangala akisema Rais
Magufuli amekuwa akitoa matamko mengi na kudai ni tofauti na ufanisi wa
Serikali yake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema
ameweka msingi mzuri katika Serikali yake, hasa kurejesha uwajibikaji na
nidhamu kwa watumishi wa umma.
“Katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi
amerejesha uwajibikaji na nidhamu jambo ambalo limejeresha hali ya kufanya kazi
ukichangiwa zaidi na utumbuaji wa majipu,” alisema Dk Bana.
Huku akipongeza kuanzishwa kwa mahakama
ya mafisadi Dk Bana alisema, “ Mwaka ujao sitarajii kuona utumbuaji majipu kwa
sababu ameshajenga msingi mzuri katika kila nyanja. Anachopaswa kufanya ni
kuongeza wigo wa upatikanaji wa ajira na kuwafanya Watanzania kuwa wazalishaji
badala ya kuendelea kuwa wachuuzi.”
Hotuba
tano
Agosti 12 mwaka huu, mwezi mmoja baada
ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli aliwataka wanachama na
viongozi wa chama hicho tawala kumvumilia kwa maelezo kuwa anataka kurejesha
heshima, imani na maadili yaliyopotea ndani ya chama hicho
“Mahali nitakapoamua kunyosha
nitanyooshea hapo hapo.
Inawezekana ujio wangu ndani ya CCM
usiwafurahishe baadhi ya watu lakini nina uhakika wanachama wetu zaidi ya
milioni nane watafurahi. Nimeamua kufanya kazi kwa uwazi ili kila pato la chama
lionekane,” alisema
Katika hafla fupi ya kumpokea
iliyofanyika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Rais alihoji
zinapokwenda fedha za viwanja 410 vya CCM, Fedha za Sukita sambamba na za jengo
la umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM), jumuiya ya wazazi, viwnaja vya mpira
na umoja wa wanawake (UWT).
Kiapo
Ikulu
Machi 7 mwaka huu katika hafla fupi ya kuapishwa kwa makatibu wakuu na naibu makatibu
wakuu 26 iliyofanyika Ikulu ilikuwa ya
aina yake kutokana na kuapa mara mbili, huku Rais Magufuli akiwaeleza kuwa
asiyeweza kazi “aseme na asile kiapo, akae kando”.
“Inawezekana tulizungumza kwa ujumla
lakini kumbe si wote wanakubali masharti kuhusu rushwa, kutoa vitu vya
upendeleo. Kwa hiyo niwaombe makatibu wakuu pamoja na kwamba mlishaapa kwangu,
ambaye hakubaliani na hilo asimame kando ili waliobaki waendelee,” alisema Rais
Magufuli kabla ya kiapo hicho.
Licha ya kauli hiyo, hakuna ahata mmoja
aliyepinga kiapo hicho.
Kuhamia
Dodoma
Julai
24 mwaka huu baada ya kuchaguliwa kuw amwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli alitangaza
ahadi kwa wanachama hao, kuwa amebakiza miezi minne na miaka minne kabla ya
kumaliza kipindi chake cha miaka mitano na kusema kabla ya kumaliza kipindi
hicho, atakuwa amehamishia serikali yote Dodoma.
Magufuli
alisema kwa sasa miundombinu ya Dodoma inawezesha serikali kuhamia huko, kwa
kuwa barabara za kutoka Makao Makuu hayo ya serikali kwenda sehemu mbalimbali
nchini, zinapitika kwa lami.
Mbali
na barabara, alisema pia huduma kwa ajili ya maisha ya watu nazo zinapatikana
kwa kuwa mkoa huo una uzoefu wa kuhudumia wabunge, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
CCM na mikutano mingine, huku mkoa huo ukiwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, ambacho
ndio kikubwa kuliko vyote nchini.
Uzinduzi
ndege ATCL
Septemba
28 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400,
Rais Magufuli aliwabeza walioziponda ndege hizo kuwa hazina kasi huku akieleza sababu za kununuliwa kwake kwa
fedha taslimu badala kulipa kidogokidogo.
Katika
uzinduzi huo, aliomba bodi na
menejimenti ya ATCL kutoruhusu kiongozi wa serikali kusafiri bure hata kama ni
yeye au waziri wa Wizara ya Uchukuzi au bodi kwani kuna wakati wanakuwa
wanajipendekeza wakati wanatakiwa kufanya biashara.
Mkutano wa wahandisi
Septemba Mosi mwaka huu wakati wa
ufunguzi wa mkutano wa mkuu wa 14 wa wahandisi, Rais Magufuli aliweka wazi
mkakati wake wa kuwadhibiti watu
wanaodaiwa kuficha fedha katika majumba yao, akiwataka kuziachia ziingie kwenye
mzunguko kwa maelezo kuwa anaweza kuamua kubadili fedha ili zinazofichwa na
watu hao wakose mahali pa kuzipeleka.
Alisema watu hao wamekuwa na utaratibu
wa kutoa fedha zao katika mabenki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi
walichonacho, kuwataka kuachana na tabia hiyo kwa sababu fedha hizo ni zao.
“Na wajiandae naweza kuamua baada ya
siku mbili tatu nabadilisha fedha na
hizo zilizofichwa katika magodoro ziozee huko…, ni nafuu mzitoe mziweke katika mzunguko zikafanye kazi.”
0 comments:
Post a Comment