Sharifa Marira na Celina Mathew
Tundu Lissu |
TAKRIBANI mwezi mmoja tangu Msaidizi wa
Masuala ya Kisiasa na Kijamii wa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Ben
Saanane atoweke chama hicho kimeibuka na kueleza kuwa hakifahamu alipo na
kuiomba Serikali ifukue makaburi ya maiti saba waliozikwa Ruvu, mkoani Pwani.
Chadema imeitaka Serikali kufukua
makaburi ya miili hiyo iliyokutwa ikielea kwenye mifuko ya sandarusi ikielea
kwenye Mto Ruvu, ili kubaini kama kuna mwili wa Saanane au la, kwani Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema ilikuwa ni miili ya wahamiaji
haramu lakini haikufanyiwa uchunguzi.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu
kupotea kwa Saanane akieleza kuwa kuna watu wanaohoji Chadema wakiitaka ieleze
alipo kiongozi huyo.
"Chadema haijui aliko Saanane,
haonekani kokote, katika mazingira haya ni vema Serikali ieleze kama vyombo vya
ulinzi vinamshikilia na kama havijamkamata mamlaka husika za mawasiliano
zieleze mara ya mwisho alifanya mawasiliano lini, wapi na nani, maana ndizo zenye
uwezo wa kuamuru mashirika ya mawasiliano kusema,” alisema Lissu.
Alisema Saanane licha ya kuwa msaidizi
wa Mbowe pia ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa kuandika vitu vya
kuikosoa Serikali na kwamba Novemba 14 ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana na
Mbowe akiwa anakwenda kwenye mazishi ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa,
Samuel Sitta.
Alisema pamoja na kwamba Saanane alikuwa
msaidizi wa Mbowe lakini alikuwa hazunguki naye mara kwa mara, isipokuwa mlinzi
wake.
“Mimi na Mwenyekiti wa Chama hatukuwa
nchini, nilirudi jana (juzi) lakini tulisoma kwenye mitandao ya kijamii kuhusu
kupotea kwa Saanane, wengine wanataka Chadema tueleze aliko, nasema hatujui
aliko, hatujui kama kafa, hajafa, katekwa au kafanywa chochote, katika hili
tunaomba Serikali itueleze aliko,” alisema Lissu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kikundi cha
vijana wanaojiita Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania, kiliiomba Chadema kuelea
aliko Saanane kikishangazwa na ukimya wa chama hicho tangu atoweke.
Lissu alisema baada ya Chadema kupata
taarifa za kupotea kwa Saanane, walishirikiana na familia yake kupeleka taarifa
Polisi na Jeshi hilo limeshafika katika ofisi hizo kufanya uchunguzi.
Alisema wiki mbili kabla ya Saanane
kupotea, aliandika kwenye mitandao ya kijamii akihoji uhalali wa Shahada ya Tatu
ya Rais John Magufuli, ambapo alipokea vitisho vingi.
Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya Rais
kuanzisha mchakato wa uhakiki wa vyeti kwa watumishi ambapo yeye aliliendeleza
kwenye mitandao ya kijamii.
Hii ni muhimu, kwa kuwa katika kipindi
cha miezi sita, watu wengine wanakamatwa kwa kuandika vibaya kwenye mitandao,
mimi nilisema dikteta uchwara nikadhibitiwa kesho yake, kuna watu 140 walikamatwa
kwa kumkosoa, hivyo hata suala hilo linaweza kuwa moja wapo.
Lissu alitaka wananchi wenye taarifa kumhusu
Saanane kuzitoa Polisi, kwa chama au kwenye vyombo vya habari, kwa kuwa hadi
sasa hakuna kinachoendelea wala taarifa zozote.
0 comments:
Post a Comment