Jacquiline Mrisho – Maelezo
Dk Charles Tizeba |
SERIKALI imesimamisha shughuli za Mfuko wa Wakfu wa
Kuendeleza Zao la Korosho ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko
huo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mfuko huo kushindwa
kutekeleza majukumu yake kikamilifu pamoja na kuwepo kwa malalamiko ya muda
mrefu kuhusu utendaji wake.
Uamuzi huo umetangazwa jana Dar es Salaam na Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu mafanikio na changamoto ya zao hilo.
Dk. Tizeba alisema kuwa lengo la uanzishwaji wa mfuko huo
lililoafikiwa na Serikali na wadau wa korosho limekuwa halifanani na
utekelezaji wake, kwani maendeleo yote yanayoonekana kwenye zao hilo hayatokani
na uwepo wa mfuko bali yanatokana na nguvu ya Serikali.
“Baada ya kutafakari utendaji wa mfuko huo tumegundua
kuwa mfuko umeshindwa kutimiza malengo yaliyodhamiriwa, umeshindwa kusimamia na
kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Bodi ya Korosho hivyo tumeamua
kusitisha shughuli za mfuko huo na kuanzia leo shughuli hizo zitatekelezwa na
Bodi ya Korosho mpaka hapo tutakapotoa maelekezo mengine.”alisema Waziri huyo.
Waziri aliongeza sababu nyingine za kusitishwa kwa Mfuko
huo ni kujihusisha na vitendo vinavyohujumu wakulima wa zao hilo hasa wakati wa
ununuzi wa pembejeo pamoja na kununua viuatilifu vilivyo chini ya kiwango kwa
bei kubwa, matumizi mabaya ya fedha kinyume cha Sheria na Kanuni za mfuko
pamoja na kushindwa kutekeleza agizo la Serikali kwa kuweka fedha kwenye amana
za muda maalumu katika Benki mbalimbali badala ya kupeleka Benki Kuu.
Aidha, Dk. Tizeba alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania anapowasilisha fedha zilizokusanywa na watu wanaosafirisha
korosho nje ya nchi kuwasiliana kwanza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho
ili kufahamu usimamizi na utaratibu wa fedha hizo.
Kwa upande mwingine, Dk. Tizeba ameizuia Menejimenti ya
mfuko huo kufanya muamala wowote wa fedha za mfuko mpaka hapo maelekezo ya
hatima yao yatakapotolewa na badala yake miamala yote itafanyika kwa utaratibu
utakaopangwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango.
Aliiagiza Bodi ya Korosho kusimamia kwa haraka jukumu la
upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu kwa sababu msimu wa zao hilo umekaribia.
0 comments:
Post a Comment