Mary Mtuka
Profesa Makame Mbarawa |
SERIKALI imeitaka Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL) kujipanga kwa mkakati wa kutangaza huduma za fedha ambazo
zitatolewa na kampuni hiyo mwakani.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua mitambo
itayotumika kwa huduma hiyo ambayo itaongeza ushindani wa biashara kwenye
huduma za simu nchini mkoani Dodoma.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari jana, Profesa Mbarawa alisema kuna umuhimu wa kampuni hiyo kujipanga
katika idara ya masoko kwa kutangaza huduma hiyo kwa njia zote.
"Ni lazima mjipange kwenye idara ya
masoko kwa kutangaza huduma yenu kwa kutumia njia zote za mitandao ya kijamii,
ili wananchi warahisishiwe huduma za fedha kupitia TTCL," alisema Waziri.
Aidha, aliitaka kampuni hiyo kujipanga
kuona fursa zilizopo kwa kutambua mahitaji ya wateja wao na kuhakikisha
inaongeza wateja mkoani humo ili kuteka soko la ushindani ambapo Serikali
inajipanga kuhamia huko.
Alisema baadhi ya maeneo ambayo TTCL
inahitaji kuboresha zaidi ni upande wa simu (voice) na data (video) ili
kurahisisha mawasiliano kwa mikutano ya njia ya video kwa kuwa baadhi ya watendaji
wengine watabaki Dar es Salaam.
"Naamini mkiimarisha mawasiliano upande
wa data mtarahisisha hata uamuzi na pia kazi zitakwenda vizuri serikalini, hasa
ikizingatiwa baadhi ya watumishi watakuwa Dodoma na wengine Dar es
Salaam," alisema.
Pia Waziri Mbarawa alisema shirika hilo
linapaswa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufikia malengo liliyojiwekea
na kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali.
Alimhakikishia Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana,
kuboresha miundombinu ikiwamo usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa Dodoma
ili kuruhusu ndege kubwa kuruka na kutua.
0 comments:
Post a Comment