Charles James
Anne Kilango Malecela |
WAKATI habari za kutumbuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Anne Kilango Malecela, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti
wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela, zikiuteka mwaka 2016
kutokana na wote kutokea familia moja, wenyewe wameibuka na kutoa neno.
Dk. Mwele ambaye alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliojitosa kuchukua
fomu za kuwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka jana, alilieleza JAMBO LEO kuwa anasita kueleza kiundani kuhusu uteuzi
wake kutenguliwa kwa sababu anachokieleza huchukuliwa tofauti.
“Naomba uniruhusu nisiongee chochote kwa sababu tangu uteuzi wangu
utenguliwe kila ninachoongea kimekuwa kikichukuliwa negative (mtazamo hasi),
hivyo naomba uniache tafadhali,” alisema Dk. Mwele.
Kutumbuliwa kwa Kilango ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu John Malecela
pamoja na mwanaye, Mwele kuliibua maswali juu ya nini kilichoikumba familia
hiyo ambayo mwaka 2016 umeshuhudia wanafamilia hao wakiondolewa katika nyadhifa
zao.
Desemba 16 mwaka huu, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Dk Mwele
baada ya kutoa ripoti ya mwaka ya taasisi hiyo iliyoonyesha kuwa watu 80 waliofanyiwa
utafiti waligundulika kuwa na virusi vya homa ya zika.
Taarifa ya utafiti huo ilionyesha kuwa kati ya watu 533
waliopimwa, 83 (asilimia 15.6) walikuwa wameambukizwa virusi vya homa ya zika,
Pia, kati ya watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu wa aina mbalimbali, asilimia
43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya homa ya zika.
Uteuzi wa Kilango ulitenguliwa siku 27 baada ya kuapishwa Ikulu
Dar es Salaam. Mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki aliondolewa katika
nafasi hiyo baada ya kudai kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa, lakini baada ya
uchunguzi kufanyika ikabainika kuwa kuna watumishi hewa 45.
Agizo la kutaka wakuu wa mikoa kusaka watumishi hewa lilitolewa na
Rais huyo wa Awamu ya Tano wakati wasaidizi wake hao wakiapa. Ilisemekana kuwa
licha ya Kilango kueleza kutokuwa na watumishi hewa ilibainika kuwa kiasi cha
Sh. milioni 339 kilikuwa kimelipwa bila kuelezwa kina nani walilipwa.
“Nimejiuliza sana, nikajiuliza sana na kwa kweli nikajiuliza sana
kwa masikitiko, kwanini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna watumishi hewa,”
alisisitiza
Rais Magufuli katika taarifa yake ya kutengua uteuzi wa Anne
Kilango.
Lakini jana Kilango alipoulizwa kuhusu hatua hiyo sambamba na yaliyoikuta
familia hiyo alisema swali hilo hakupaswa kuulizwa jana kwa sababu alikuwa
katika Sikukuu ya Krismasi.
“Mimi nipo kwenye Krismasi naandaa pilau la sikukuu, naomba uniache,”
alisema Kilango.
0 comments:
Post a Comment