*Baadhi
waona yatabana matumizi, kuleta ufanisi
*Wengine
wasema huenda yakasababisha mpasuko
Waandishi
Wetu
SIKU moja baada ya CCM kufanya
mabadiliko makubwa kwenye muundo wake kwa kupunguza vikao na idadi ya wajumbe
wa ngazi zote, wasomi na wanasiasa wameuchambua mwonekano huo mpya na
kubainisha faida na hasara zake, ikiwemo ya kuibuka mpasuko na ajira kuota
mbawa.
Wamesema mabadiliko hayo yanaweza kukiathiri
au kukinyanyua chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na
Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, huku aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila akihoji sababu za Rais John Magufuli kuendelea kuwa na kofia mbili za urais
na uenyekiti wa chama, huku akitaka wana CCM kuwa na nafasi moja tu ya uongozi.
Mabadiliko hayo 23 ya CCM yalipitishwa kwenye
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho juzi Dar Salaam chini
ya Rais Magufuli, yakishuhudia kupunguzwa idadi ya wajumbe na idadi ya vikao
vya chama, sambamba na kuondolewa kwa vyeo ambavyo haviko kwenye Katiba.
Wakati baadhi wakisema mabadiliko hayo yataokoa
matumizi ya fedha na hivyo kubana matumizi, kuondoa urasimu, msuguano kwenye
vikao, wataalamu waliokosa ajira CCM kurejea katika taaluma zao, kuondoa watu wasiokuwa
na shughuli za msingi.
Wengine waliponda kuwa CCM itatetereka
kwa kufuta nyadhifa za wajumbe wa wilaya na mikoa, kupunguza idadi ya vikao,
kuondoa makatibu wa jumuiya zake na kukitabiria mpasuko baada ya kutosa wajumbe
na wanachama kukosa ajira
“Hali ya uchumi kwa sasa si nzuri, hivyo
kuendelea kuwa na idadi ya wajumbe wengi ni kuongeza gharama za uendeshaji wa chama.
Kilichofanyika kimelenga kubana matumizi makubwa,” alisema Dk George Kahangwa,
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Udassa).
“Unajua kuna kundi kubwa la watu
walikuwa wamekimbilia kwenye siasa na kuacha taaluma zao, zile nafasi
zilizofutwa ndani ya CCM tutarajie kuona wahusika wakirejea kwenye taaluma zao,
huenda wamo walimu, madaktari na hata watafiti.”
Akizungumzia kupunguzwa kwa wajumbe 288
hadi 158 wa NEC, Dk Kahangwa alisema: “Hata kiungo kikiwa mwilini na hakifanyi
kazi ukikiondoa si tatizo. Ila kufyekwa kwa wajumbe wa kamati za siasa za mikoa
na wilaya kutaongeza watu wasio na ajira mitaani.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda alisema: “Mabadiliko yaliyofanyika yatapunguza matumizi
ya fedha kwenye vikao ambavyo sasa vitafanyika vichache. Ila kupungua kwa idadi
ya wajumbe pia kutaifanya CCM iokoe posho na mishahara iliyokuwa ikiwalipa.
Fedha hizo sasa zitasaidia mambo mengine.”
“Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati
Kuu waliopunguzwa wanaweza kuamua kwenda Upinzani, au kuunga mkono Upinzani
wakiwa ndani ya CCM, baada ya kutofurahishwa na mabadiliko. Hilo linaweza kuwa
pigo kwa chama hicho tawala,” alisema Mbunda.
Hamad Salim wa Chuo Kikuu Huria (OUT) aliungana
na Mbunda kuhusu CCM kubana matumizi zaidi baada ya kupunguza idadi ya wajumbe
wa vikao na kupunguza wajumbe wa mikoa na wilaya.
“Pia uchache wao katika vikao utasaidia
kupitisha uamuzi haraka bila mvutano. Nadhani utakumbuka wakati wa mchakato wa
CCM kupata mgombea wake wa urais. Mvutano ulikuwa mkali kutokana na sababu nyingi,
ikiwamo ya wingi wa wajumbe kwenye vikao,” alisema Hamad huku akipongeza uteuzi
wa Humphrey Polepole kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, kwa maelezo kuwa ni
mahiri katika siasa.
Kauli hiyo ya Hamad ilipingwa na Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju kwa maelezo kuwa vikao kuwa na wajumbe
wachache ni rahisi kwa Mwenyekiti kuwamudu na kuweka wajumbe anaotaka.
“Kikwete (Jakaya-Rais mstaafu) aliweka
utaratibu wa wajumbe wengi ili kuondoa rushwa kwa wingi wao. Hivi sasa wajumbe
wa NEC wameondolewa 230 na kubaki 158, hii inaleta picha kuwa huenda hata
watendaji wa Serikali waliondolewa na Rais Magufuli kimkakati ili kuweka
wanaotekeleza matakwa yake,” alisema Juju.
“Si mfumo sahihi sana, pia kupunguzwa
kwa idadi ya vikao si sahihi, kwa kigezo cha kutaka watu wafanye kazi, hivi
utafanya kazi za siasa bila vikao?”
Katika ufafanuzi wake, Kafulila alisema:
“Hoja ya Rais Magufuli kutenganisha kofia mbili kwamba mawaziri na wabunge
wasiwe viongozi wa chama ni jambo la jema sana kimfumo, bahati mbaya amesahau
kwamba ilitakiwa utekelezaji wake uanze na yeye mwenyewe kuacha uenyekiti wa
chama ili abaki kuwa Rais.”
Kafulila ambaye aliibua sakata la Tegeta
Escrow na kusababisha viongozi kadhaa wa Serikali kujiuzulu, aliponda uteuzi wa
Kanali Ngemela Lubinga kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa, kwa maelezo kuwa uamuzi huo unaleta picha kuwa ndani ya Jeshi kuna
makada wa chama hicho.
Kisena Mabuba, Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), aliungana na baadhi ya wachambuzi
kwamba mabadiliko hayo yataondoa msuguano na gharama za uendeshaji vikao.
“Napongeza kuondolewa kwa vyeo ambavyo
si vya msingi na kuvunja Katiba ya Chama hicho. Ila CCM wasidhani kuwa mfumo
huu mpya utaondoa rushwa. Watafute njia mbadala ya kukabiliana na rushwa,”
alisema.
Izack Mponeka ambaye kitaaluma ni
mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Maendeleo ya Jamii alisema, “kuondolewa kwa makatibu
wa jumuiya za CCM kunapaswa kuangaliwa upya kabla ya utekelezaji.”
“Nasema hivi, kwa sababu wamekuwa
wakifanya kazi kubwa bila msaada wa makatibu wa chama, hali ambayo ilikuwa changamoto
kwa jumuiya hizo kuonesha ufanisi.”
Mhadhiri wa UDSM, Dk James Jesse aliunga
mkono kupunguzwa kwa wajumbe wa vikao kwa maelezo kuwa wachache wataleta
ufanisi zaidi.
Imeandikwa
na Fidelis Butahe, Suleiman Msuya na Charles James
0 comments:
Post a Comment