*Asema atakuwa mkweli daima fitina kwake mwiko
*Nape
akunja uso, aomba radhi wote aliowakosea
Fidelis Butahe
Humphrey Polepole |
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec)
ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amekubali madaraka ya usemaji wa
chama hicho, huku aking’ang’ania msimamo wake wa Muungano wa Serikali Tatu,
unaopingana na matakwa ya chama hicho.
Polepole alitoa msimamo huo jana kwenye
ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, alipokuwa akijibu maswali
ya waandishi wa habari mbele ya mtangulizi wake, Nape Nnauye aliyeonekana
kutoridhishwa sana na majibu hayo.
Hata hivyo, Nape alipotakiwa
kumzungumzia mrithi wake, alimsifu akisema hana shaka na uadilifu, uzalendo,
uwezo, usasa na ujana wake na kwamba huenda ndiyo miongoni mwa sifa zilizochangia
uteuzi wake.
Ukweli daima
Akijibu maswali ya waandishi wa habari
wakati akitambulishwa na kukabidhiwa ofisi na Nape, Polepole alisema msimamo
wake kuhusu kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi kwenye mchakato wa Katiba Mpya uko
palepale, akisisitiza, “nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.”
Huku akizungumza kwa umakini na
kujiamini, Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu Joseph Warioba, alisema kwa kuwa
aliamini maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Tume ambayo yaliondolewa kwenye
Katiba Inayopendekezwa, ataendelea kuamini hivyo na kusisitiza kuwa yeye si mtu
wa kubadili maneno.
Miongoni mwa misimamo ya kada huyo wa CCM
kuhusu mchakato huo, ni pamoja na kutaka muundo wa Muungano wa Serikali Tatu
badala ya mbili, Rais kutoteua wabunge, sifa za elimu kwa wabunge, nafasi za makatibu
wakuu na naibu makatibu wakuu kuwekwa kikatiba pamoja na haki ya kutokuwa
mtumwa, uhuru wa habari na vyombo vya habari na haki mbalimbali.
Kuhusu serikali tatu, Polepole aliwahi
kukaririwa akisema: “Mpango wa CCM kuingiza ajenda ya serikali mbili ndani ya
rasimu ya Katiba, utaiingiza nchi kwenye matatizo. Hii ni kwa sababu, serikali
mbili ndani ya Muungano hazitekelezeki.”
Mambo hayo yote pamoja na mengine
yaliyowahi kunukuliwa na kada huyo, yaliondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa,
ambayo mchakato wake wa kuipigia kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’, ulisimama tangu
Aprili mwaka jana, kupisha Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, Novemba 4 alipozungumza na
wahariri wa vyombo vya habari, Rais John Magufuli alisema hakuwahi kuzungumzia
Katiba wakati wa kampeni zake, kwa hiyo si kipaumbele chake na kwamba
anachotaka kwanza ni “kunyoosha nchi”, jambo lililoashiria kuwa mchakato
umesimama kwa muda usiojulikana.
Katika swali hilo, Polepole aliulizwa
kama ataendelea na msimamo wake wa kuamini muundo wa Serikali Tatu; Serikali ya
Tanganyika, Zanzibar na Muungano; huku msimamo wa CCM na uliomo kwenye Katiba
Inayopendekezwa iliyopitishwa na wabunge wa chama hicho, ikitaja mfumo uliopo
sasa wa serikali mbili.
“Mimi ni mwanachama wa CCM kwa imani na
ninaziishi ahadi za chama na mojawapo ni kusema kweli daima na fitina kwangu ni
mwiko.
“Msimamo wangu ni madhubuti kwenye chama
changu na Taifa langu. Iliyo haki nitasimamia haki, iliyo kweli nitaisema kweli
wakati wote na huwa sibadilishi maneno, ahsante sana,” alisema Polepole.
Kabla ya kueleza msimamo wake huo,
Polepole alibanwa kwa swali lingine lililomtaka aeleze msimamo wake kuhusu
mchakato huo; kwamba uendelee ulipoishia au urejeshwe kwa maoni ya wananchi
yaliyofutwa.
“Sidhani kama kuna mkwamo. Mchakato huu
umeahirishwa kwa mazingira ambayo yalikuwa wazi, hata Rais Magufuli
ameshalisemea hili, sasa Rais anatunyooshea kwanza nchi kupata utamu wa yale
tunayotaka. Wakati ukifika usiwe na shaka, jambo hili lipo kwenye mikono salama
chini ya Rais Magufuli,” alisema.
Maridhiano
Alisema mchakato wa Katiba ni muhimu kwa
Taifa na unahitaji mwafaka, maridhiano na uelewa, hatua iliyoonekana kuachwa
wakati Katiba Inayopendekezwa ilipopitishwa kwa kura.
“Rais ana mwaka mmoja madarakani, anapanga
nchi na chama…nafikiri mabadiliko ndani ya CCM na ukitazama kwa sura kubwa misingi
ya uadilifu, miiko ya uongozi, uwajibikaji na huduma bora vinavyosimamiwa sasa,
utaona dhamira ya Serikali ya CCM kuelekea huko (kupata Katiba),” alisema.
Polepole pia aligusia misingi ya
kuanzishwa kwa chama hicho, huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii, ili CCM ipate
wanachama wengi zaidi.
“Tutataka kufundisha wananchi na watu
wenye mapenzi mema kuhusu misingi ya chama chetu na hasa imani yake. Kama sisi
wanachama wa CCM tukiiishi misingi ya chama hata kwa asilimia 60, hii nchi
haitachukua muda mrefu kufika tunakotaka,” alisema.
Kukosoana
Alisema lazima CCM ishughulike na shida
za watu na mtaji wake uwe ni wanachama na Watanzania, “tufanye siasa za
maendeleo na tupunguze siasa za madaraka… kukosoana ni sehemu ya msingi.”
Awali, Nape ambaye alionekana kukunja
uso wakati Polepole akielezea msimamo wake, aliishukuru CCM kwa kumwamini na
kumpa nafasi ya uongozi kwa miaka mitano, huku akimmwagia sifa Katibu Mkuu wa Chama
hicho, Abdulrahman Kinana na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
“Kama kuna kitu nitakikosa CCM ni kufanya
kazi na Kinana. Amenitengeneza kufika hapa nilipo leo. Amekijenga chama na
kunilea. Wakati naingia hali ya chama ilikuwa ngumu kidogo, ila kwa ushirikiano
wake na wanachama wenzangu tumefika tulipofika.
Siri
“CCM ni zaidi ya shule. Nafikiria baada
ya kustaafu nafasi hii, nitaandika kitabu cha kueleza ukatibu uenezi wangu
ulivyokuwa. Yapo mambo mengi sijayasema na hayajasemwa na mtu yeyote,
nitayazungumza kwa faida ya wengine,” alisema Nape.
Pia alitumia nafasi hiyo kuomba radhi
aliowakosea, wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani nchini.
“Watani zangu tumetupiana maneno na
vijembe, lakini nia ilikuwa njema kuijenga Tanzania yenye siasa nzuri,
ushindani na hoja. Katika hali ile tumekanyagana hapa na pale, binafsi nimewasamehe
lakini nao naamini wamenisamehe nilipowaumiza, haikuwa nia yangu,” alisema
Nape.
Akimzungumzia Polepole, Nape alisema:
“Sina shaka na uadilifu, uzalendo, uwezo, usasa na ujana wake. Nadhani hizo ni
miongoni mwa sifa zilizowafanya wale walioamua kumteua kuchukua nafasi hii. Anatosha.”
0 comments:
Post a Comment