Abraham Ntambara
WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuchangia damu, ili kusaidia kuokoa
maisha ya wagonjwa wa dharura ambao ni majeruhi, wajawazito na watoto.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es
Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Makwaiya
Makani wakati wa uzindizi wa kampeni ya uchangiaji damu wa madereva bodaboda
unaoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la APEC.
“Damu ni uhai, haipatikani viwandani,
kila mmoja anaweza kuwa na uhai wa mwingine kwa kuchangia damu,” alisema
Makani.
Aliwaambia madereva hao kuwa uchangiaji
damu ni suala la muhimu katika kuokoa maisha ya wengine na kubainisha kwamba
duniani kote wapo watu huokolewa kwa kuchangiwa damu na watu ambao hawajawahi
kukutana nao.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema hospitali
hiyo inahitaji chupa za damu 120 kwa mwezi, lakini wamekuwa wakiishia kupata
chupa 80 huku kukiwa na upungufu ya chupa 40 jambo linalofanya wahudumie
wagonjwa wa dharula tu huku wengine wakishindwa kuhudumiwa.
Alibainisha kuwa kwa kawaida damu
huhifadhiwa kwa takribani mwezi mmoja tu na baada ya hapo huisha muda wa
matumizi na kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakihamasisha uchangiaji wa damu
mara kwa mara.
Alisema upatikanaji wa damu kwa wakati
husaidia kuokoa maisha na uchangiaji wa hiari wa damu ndiyo msingi wa
upatikanaji wa damu bila malipo.
Mkurugenzi wa APEC, Respicius Timenywa
alisema wao ni miongoni mwa waaanzilishi wa huduma ya bodaboda nchini na
wamekuwa wakizunguka kuhamasisha uchangiaji wa damu nchi nzima.
“Kutokana na ajali nyingi za bodaboda,
mwaka huu tumeamua kuhamasisha bodaboda kuchangia damu, ili kuokoa maisha ya
wenzao,” alisema Timanywa.
Timanywa aliiomba Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuunga mkono
shirika hilo kwa kulipa gari mbili aina ya Land Cruiser zitakazowasaidia
kuzunguka nchi nzima kuhamasisha uchangiaji damu, ili watimize lengo
walilojiwekea la kukusanya mililita 500 za damu kwa kila mwezi.
Meneja wa Damu Salama Kanda ya
Masahariki, Dk. Avelina Mgasa alisema takwimu zinaonyesha kuwa wajawazito na
watoto ndio waathirika wenye uhitaji mkubwa wa huduma ya damu.
Alisema ni jukumu la kila mdau
kuhakikisha damu salama inapatikana na kuongeza kuwa damu ni uhai na
haipatikani kwa njia nyingine bali kwa binadamu pekee.
Alisisitiza kuwa damu inatakiwa kutolewa
bure kwa wagonjwa na kuwataka wananchi kutoa kutoa taarifa za watumishi wanaowataka
wagonjwa kutoa fedha ili kupatiwa huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment