Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi imetupilia
mbali maombi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ya kutaka kurudishwa
kwenye jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) 'Billicanas', kutokana na
kudaiwa kodi ya Sh bilioni 1.3 na shirika hilo.
Uamuzi huo wa kutupwa kwa maombi ya Mbowe uliosomwa kwa
saa moja ulitolewa jana na Jaji Sivangilwa Mwangesi, baada ya kupitia hoja
mbalimbali na mawakili wa Mbunge huyo na wa NHC.
Jaji Mwangesi alisema baada ya kupitia hoja zao za awali
alijiridhisha kwamba mchakato wa kumhamisha Mbowe kutoka jengo hilo ulifanyika
kihalali.
Alisema mchakato huo ulioendeshwa na kampuni ya udalali
ya Foster Auctioneers and General Traders, ulikuwa halali na ulifuata taratibu
zote za kisheria.
“Kampuni hii ilifuata taratibu zote za kisheria tofauti
na ilivyodaiwa na upande wa mlalamikaji, pia kuhusu suala la mkataba baina ya
Mbowe na NHC, hilo si sehemu ya Mahakama.
“Kutokana na kujiridhisha huku, Mahakama inatupilia mbali
maombi ya Mbowe ya kutaka kurudishwa kwenye jengo la Billicanas," alisema
Jaji Mwangesi.
Jaji huyo alisema alitupilia mbali maombi hayo bila gharama,
kwa hiyo Mbowe hatatakiwa kulipa gharama za maombi hayo.
Mbowe kupitia kampuni yake ya Mbowe Hotels Limited,
alifungua shauri namba 722 la mwaka 2016 dhidi ya NHC, akiiomba Mahakama itoe
amri ya kurejeshwa katika jengo hilo, kwa madai kwamba kuondolewa kwake
kulifanywa kinyume cha sheria.
Kupitia mawakili wake, alidai hakupewa ilani na NHC kumtaarifu
kwamba anapaswa kuondoka kwenye jengo hilo na kwamba aliondolewa bila amri ya Mahakama.
Pia aliomba arudishiwe mali zake zilizochukuliwa na NHC
kupitia kampuni ya udalali ya Foster, kwa maelezo kwamba zilichukuliwa kiholela
huku wakidai kuwa kampuni hiyo ya udalali haikusajiliwa na Mahakama na pia aliiomba
itolewe amri ya kuzuia asibughudhiwe baada ya kurudishwa.
Katika madai ya msingi ya Mbowe, Wakili Kibatala alidai kuwa
mteja wake si mpangaji kwenye jengo hilo, bali ni mbia ambaye anamiliki
asilimia 75 katika uendeshaji wake huku NHC wakimiliki asilimia 25.
Msingi wa pili, Kibatala aidai kuwa hata kama Mbowe
angekuwa anadaiwa kodi na NHC, kuondolewa kwake kulifanywa bila kuzingatia
sheria, kwa kuwa hakukuwa na amri ya Mahakama iliyowapa wadai nguvu ya kisheria
ya kumwondoa.
Kwa upande mwingine, Mbowe kupitia hati ya kiapo, alidai kuwa
hadaiwi hata senti tano na NHC kama pango la jengo la Billicanas na kwamba
amekuwa akilipa tozo zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mkataba baina yake na
shirika hilo.
Nje ya Mahakama
Baada ya uamuzi huo, hali ilikuwa tete kwa mawakili wa
Mbowe, Peter Kibatala, John Mallya na Omary Msema kwa kuona kuwa Mahakama hiyo
haikutenda haki kwa mteja wao kwa hiyo watakata rufaa.
Wakili Mallya alisema walipokea uamuzi na waliiomba Mahakama
iwape nakala ya uamuzi na kwamba jambo hilo halitaishia hapo litakwenda mahakama
za juu.
“Tutakata rufaa na tutakwenda mahakama za juu, hivyo
tutaupitia vizuri uamuzi huu kisha tuchukue hatua, hivyo mkataba wa Mbowe na
NHC haukupata kutekelezwa na haupo,” alisema Mallya.
Kibatala alisema wamepeleka maombi ya nakala ya uamuzi
huo ili waende kwenye marejeo katika Mahakama ya Rufaa na pia wamepeleka maombi
ya kuzuia chochote kufanyika katika eneo husika.
Akizungumzia mali za Mbowe, alisema hadi watakapopata
uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, baada ya kupitia uamuzi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kitengo cha Ardhi.
NHC
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa NHC, Aliko Mwamanenge
alisema wanaishukuru Mahakama kwa kutenda haki kutokana na uamuzi huo.
Alisema kutokana na uamuzi huo Mahakama ilikubali kwamba
kila kitu kilichofanyika siku ya kutolewa kwa mali za Mbowe kilifanyika
kihalali, hivyo mali zake haziwezi kurudishwa.
"Mali zake haziwezi kurudishwa kwa sababu bado
hajalipa deni analodaiwa na shirika, kwa hiyo atapewa mali zake atakapolipa
deni hili,” alisema Mwamanenge.
0 comments:
Post a Comment