*Wamo Lissu, Lipumba, waliokuwa vigogo TRA
Grace
Gurisha
WAKATI
mwaka 2016 ukielekea ukingoni, Watanzania wanakumbuka kesi kumi kubwa
zilizotikisa mwaka huu wa kwanza wa utawala wa Rais John Magufuli.
Uchunguzi
umebaini kuwa Watanzania wengi hasa wa mijini, wamejadili kesi ya aliyekuwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake na
kesi ya aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato (TRA),
Tiagi Masamaki na wenzake.
Kesi
zingine zilizovuta hisia za watu wengi mwaka huu ni Mpemba wa Magufuli (Yusuf
Yusuf), mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo, mfanyabiashara bilionea
aliyetajwa na Rais Magufuli kuwa anajipatia fedha kati ya Sh milioni saba kwa
dakika moja, Mohamed Yusufali ambaye alipandishwa kizimbani kwa makosa ya
kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya bilioni 14.
Pia,
mwaka huu kulikuwa na kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Vitambulisho (Nida), Dickson Maimu, Profesa Lipumba na Maalim Seif, kesi ya
uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kesi ya aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji Kipallo Kisamfu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ‘mabehewa
feki’, kesi ya wabunge wa CCM kizimbani kwa rushwa na Zombe kufutiwa kesi ya
mauaji.
Kesi Kitilya
Kitilya
na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam wakishitakiwa kwa makosa la Uhujumu Uchumi, likiwemo la kutakatisha
fedha haramu na kujipatia isivyo halali dola za Marekani milioni 6, sawa na sh
bilioni 12.
Mawakili
wake walipigana kufa na kupona ili mteja wao aondolewe kosa la kutakatisha
fedha, lakini ilishindikana, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa
uamuzi kuwa shitaka hilo liko kihalali katika hati ya mashitaka.
Kutokana
na hali hiyo Kitilya bado anaendelea kusota rumande kwa sababu upelelezi wa
kesi hiyo bado haujakamilika.
Kesi ya Masamaki
Kesi ya
Masamaki maarufu kama kesi ya makontena ilitikisa nchi kutokana na taarifa
ambazo zilikuwa zinazagaa kuwa tajiri huyo ana nyumba zaidi ya 70 na pia ndani
ya nyumba yake aliyokuwa akiishi, alikutwa na mabilioni ya fedha.
Hata
hivyo, Masamaki na wenzake waliachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu, baada ya
kutimiza masharti waliyopewa. Bosi huyo huyo yupo nje na upelelezi wa kesi yake
bado haujakamilika.
Mpemba wa Magufuli
Yusuf
Yusuf maarufu kwa jina la Mpemba, alipandishwa kizimbani, baada ya Rais
Magufuli kumtaja hadharani kuwa ni kinara wa ujangili wa kujihusisha na
biashara ya meno ya tembo. Mwenyewe amekana kosa na upelelezi wa kesi yake bado
haijakamilika.
Bilionea Yusufali
Mfanyabiashara
bilionea aliyetajwa na Rais Magufuli kuwa anajipatia fedha kati ya Sh milioni
saba kwa dakika moja, Mohamed Yusufali alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuisabishia
Serikali hasara ya Sh bilioni 15 kwa kukwepa kodi.
Yusufali
bado anaendelea kusota rumande kwa sababu upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika
kutokana na kwamba katika makosa 199 yanayomkabili, moja ni la kutakatisha
fedha haramu ambalo kisheria halina dhamana.
Maimu
Siku
chache tu baada ya Rais Magufuli kueleza uchafu uliyoko ndani ya Nida,
Mkurugenzi wa Mashitaka aliwaandalia mashitaka Maimu na wenzake, akituhumu
kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja kwa kutumia mamlaka
yao vibaya.
Kesi
hiyo imeanza kusikilizwa, baada ya upelelezi wake kuchukua muda mrefu
kukamilika.
Profesa Lipumba na Maalim Seif
Bodi ya
Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) kilifungua kesi katika Mahakama Kuu dhidi
ya Lipumba na wenzake na kuiomba Mahakama hiyo itengue barua ya Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi iliyomtambua Lipumba kuwa mwenyekiti wa
chama hicho.
Watu
wengi wanataka kujua mwisho wa kesi hiyo kutokana na nguvu ya Profesa Lipumba katika
siasa za upinzania. Kesi hiyo ipo katika hatua ya kuanza kusikilizwa.
Zombe huru, Bageni kunyongwa
Kuachiwa
huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe kulizua maswali mengi sana kwa
Watanzania wengi kutokana na kwamba tayari wao walishamuhukumu kutokana na sifa
ambazo alikuwa nazo.
Wengine
walifikia hatua kusema anatumia nguvu za giza kutokana na hukumu ambayo
ilitolewa ya yeye kuachiwa na aliyekuwa bosi wa Jeshi la Polisi, Christopher
Bageni kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Kesi hii
ilikuwa inawasimumua watu wengi kutokana na umaarufu wa Zombe katika kazi ya
Jeshi la Polisi aliyokuwa akifanya, kwa hiyo watu walitegemea Zombe ndiyo
atafungwa na sio Bageni kwa sababu Bageni alikuwa anafuata maagizo ya bosi
wake.
Kisamfu
Kisamfu
alipandishwa kizimbani na vigogo wengine 10 akituhumiwa kutumia vibaya madaraka
yake kwa kushindwa kusimamia vizuri zabuni kama ilivyokuwa inatakiwa kwenye
vigezo vya masharti na kusababisha kununuliwa kwa mabehewa 25 ambayo hayana
ubora.
Kesi
hiyo ilipelekwa mahakamani baada ya Waziri husika kupiga kelele baada ya
kubaini kuwa mabehewa hayo yalikuwa chini ya kiwango.
Melo
Kesi ya
kushindwa kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu ya upelelezi
inayomkabili Melo ilizua utata mkubwa katika tasnia ya habari kutokana na
kwamba alikuwa akishinikizwa kutoa taarifa za kieletroniki ambazo zilikuwepo
kwenye mtandao wa Jamii Forums ambao anaouendesha.
Hali
hiyo ilisababisha Melo kukaa mahabusu zaidi ya siku tano, kitu ambacho
kilisababisha hofu kwa watu wengi ambao walikuwa wanachangia katika mtandao huo
wa kijamii.
Baadaye
Melo aliachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Makazim Kisutu, Dar es Salaam,
baada ya kukaa mahabusu siku sita akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
mahojiano.
Lissu
Lissu
alipandishwa mara tatu kizimbani akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi, likiwemo
la ‘dikteta uchwara’. Jamii imekuwa ikifuatilia kesi hiyo hasa ilipoelezwa kuwa
hata pale ambapo alishindwa kutokea mahakamani bila taarifa, mamlaka husika zilishindwa
kumkamata, licha ya mahakama kutoa hati ya kumkamata.
Hali
hiyo ilizidi kumpaisha Lissu katika kesi zake, ambapo kila mtu alitamani kujua
kinachofuata. Kesi hizo zimeanza kusikilizwa, huku Mbunge huyo akionekana
kujiamini.
0 comments:
Post a Comment