Stella Kessy
Edwin Ngonyani |
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Edwin Ngonyani, ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads)
mkoani Morogoro kuhakikisha wanafanya matengenezo katika barabara zao ili
zipitike katika kipindi chote cha mwaka.
Ngonyani alisema jana katika taarifa
yake kuwa hilo limeanza kutekelezwa katika barabara ya Ifakara, Taweta hadi
Madeke yenye urefu wa km 225) na barabara ya Ifakara kwenda Kihansi ya km 130
ambako upembuzi yakinifu umeshafanyika.
"Katika miaka hii mitano
tutahakikisha maandalizi ya awali ya kuwezesha barabara hii kujengwa kwa kiwango
cha lami yanakamilika na hivyo kutuwezesha kutenga fedha kwa ajili ya kuanza
ujenzi rasmi," alisema.
Alisema kuwa barabara hiyo ni kiungo
muhimu kwa wakazi wa Ifakara na Kilombero kwa kuunganisha na mkoa wa Njombe na
hivyo kukamilika kwake zitafungua fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi
hao.
Ngonyani amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano itaendelea kutekeleza ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi kwa kuunganisha
mikoa mbalimbali kwa ujenzi wa barabara bora za viwango vya lami ili
kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.
"Serikali ya awamu ya tano ipo
madarakani kwa ajili ya wananchi bila kujali itikadi zao, tumewaahidi kuwaletea
maendeleo hivyo tutajenga barabara zote tulizoahidi kwa wakati ili wananchi
waendelee kunufaika na matunda ya serikali yao,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia wizara
yake itaboresha huduma za mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi ili kuwawezesha
wananchi kuwasiliana wakati wowote ili kukuza mahusiano yao kiuchumi,
kibiashara na hivyo kukuza pato lao na la taifa.
"Tumeuomba uongozi wa kila wilaya
utuletee maeneo ambayo huduma za mawasiliano hazijafika au zinasumbua ili sisi tuweze
kuzishughulikia na kuzipatia huduma bora za mawasiliano,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la
Mlimba, Suzani Kiwanga ameishukuru serikali kwa uamuzi wa kuiweka barabara hiyo
katika mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami kwa kuwa itafungua fursa
mbalimbali kwa wananchi ambao wataweza kusafirisha mazao yao kwenda katika
sokoni kwa urahisi.
0 comments:
Post a Comment