Salha Mohamed
Paul Makonda |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani mwake, kutokubali kubomolea nyumba
wananchi bila kujiridhisha kwa hukumu halali za Mahakama.
Pia Jeshi la Polisi limetakiwa kutosimamia
mchakato wa ubomoaji nyumba bila Mkuu wa Wilaya kujiridhisha na uhalali wa
kubomoa.
Makonda alisema hayo jana wakati akimwapisha
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori aliyechukua nafasi ya Humphrey Polepole
aliyeteuliwa kuwa Katibu Mwenezi wa CCM.
Alisema kuna tabia mkoani humo ya watu
kutekeleza hukumu za Mahakama na zingine zikiwa feki kwa kubomolea wananchi
nyumba zao.
“Hakuna mtu anayeruhusiwa kubomoa nyumba
bila ninyi (wakuu) kujiridhisha kwamba ana hukumu halali ya Mahakama, kama hana
hukumu halali una nafasi ya kuchukua hatua,” alisema huku akibainisha kutumia
wanasheria wa mkoa na manispaa hizo kupitia nyaraka zote.
”Kwa hiyo wale wote sijui Majembe Auction
… hawaruhusiwi kubomoa nyumba hadi DC uwe na uhakika kwamba hatua za hukumu
zimepitishwa kihalali,” alisema.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuzuia
kilio cha wanyonge na masikini ambao wanabomolewa nyumba na baada ya siku
inagundulika kuwa hukumu ni bandia.
“Nawaagiza wakuu wa wilaya simamieni
hilo, ili mwakani tuongeze kasi ya kutetea wanyonge. Hakuna mtu mwenye mamlaka
ya kubomoa nyumba kama wewe hujaridhika,” alisema.
Makonda aliitaka Polisi kutoshiriki
mchakato wa kuvunja nyumba za wananchi hadi DC atakapojiridhisha.
Makori, alisema anatambua wilaya hiyo
ina changamoto nyingi za huduma za maendeleo wanayohitaji.
“Viongozi nitakaokuwa nao katika
majukumu haya, tushirikiane kuhakikisha tunatatua kero na matatizo ya nchi,
kwani siasa nzuri ni ya kuleta maendeleo na kubadilisha maisha ya watu yawe
tofauti na yalivyo sasa,” alisema.
Aliwahakikishia wananchi kuwa na nia ya
kufanya kazi na si porojo na kufanya mambo yatakayoleta ahueni kadri fursa itakapojitokeza
kwa wananchi wa Ubungo kuona tofauti.
0 comments:
Post a Comment