Hussein Ndubikile
ZIKIWA zimebaki siku tatu kusherehekea
Sikukuu ya Krismasi, abiria wa mabasi yaendayo mikoani wamekwama kwenye kituo
cha mabasi ya mikoani cha Ubungo, Dar es Salaam na kulazimika kutumia usafiri
wa daladala aina ya Eicher kwenda mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye
kituo hicho ulibaini kuwapo kwa daladala hizo zilizokuwa na abiria wakielelea
mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Kagera.
Dereva wa moja ya mabasi hayo, Rashid
Msangi alisema huduma ya usafiri wa mabasi kituoni hapo imeadimika kutokana na
abiria kuongezeka kuanzia juzi (Jumanne) na jana,
hali iliyosababisha kuomba vibali na kukaguliwa na wakaguzi wa kikosi cha
polisi wa usalama barabarani.
"Abiria wameongezeka, juzi walianza
kuondoka na daladala hizi leo (jana) ndio kama unavyowaona hawa, wanaelekea
Arusha na Moshi," alisema.
Alisema kwa safari za mikoa hiyo
huwatoza nauli ya kati ya Sh 25,000 na Sh 28,000 kufuatana walivyoelekezwa na
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Chama cha
Kutetea Abiria nchini (Chakua).
Wakala wa kampuni ya Happy Nation,
Swalehe Yasin alisema tatizo hilo limetokea kwa watu wa mikoa hiyo kutosafiri
mapema kama ilivyozoeleka, huku akiongeza kuwa ugumu wa maisha nao umechangia
hali hiyo.
Yasin alisema tiketi za mabasi
yanayokwenda mikoa hiyo zimekwisha, hivyo kwa abiria anayehitaji anatakiwa
kwenda kituo hicho cha mabasi Jumapili.
Abiria Hassan Issa aliyekuwa akielekea
Arusha alisema alifika kituoni hapo saa 2 asubuhi na kukuta mabasi yamejaa hali
iliyomlazimu kusubiri usafiri wa daladala hizo.
Abiria wa Korogwe, Tanga, Mwanakhamisi
Ramadhan alisema alipata adha kubwa ya usafiri kutokana na mabasi kuwa machache
na aliyoyakuta kujaa abiria.
Ofisa Elimu wa Chakua, Gervas
Rutaguzinda alisema uhaba wa mabasi umetokana na idadi ya abiria kuongezeka na kulazimika
kutafuta njia mbadala ya kusaidia abiria wanaokwenda mikoa hiyo kwa kuleta
daladala zinazofanya safari za Gongo la Mboto, Tegeta, Mbagala na Kibaha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga kikosi chake imejipanga kudhibiti
ajali za barabarani kwa kuongeza askari na utozaji wa nauli wa kiholela.
Kamanda Mpinga alisema daladala
zinazobeba abiria Ubungo hazifanyi safari bila kukaguliwa na wakaguzi wa kikosi
hicho.
0 comments:
Post a Comment