*Nia ni wafanyabiashara wakwepa kodi wabanwe
*Ampongeza
JPM asema hakuna haja ya upinzani
Mwandishi Wetu
Mustapher Jaffar Sabodo |
WAKATI wananchi wakilia ukata mifukoni
kwa madai fedha zimetoweka kwenye mzunguko, mfanyabiashara maarufu nchini,
Jaffar Sabodo (73), amemshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha ili kubana
wafanyabiashara wakwepa kodi na kuficha fedha majumbani.
Aidha, amesema kutokana na utendaji wa Rais,
haoni sababu za vyama vya upinzani kuendelea kumpinga, na badala yake waache
siasa na waungane naye kujenga Tanzania mpya.
Kauli ya mfanyabiashara huyo iliungwa
mkono na wachumi waliozungumza na gazeti hili kubainisha kuwa njia nzuri zaidi
ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kupunguza masharti kwa benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe
kubwa jambo ambalo litafanya watu wakiweka fedha benki wapate faida.
Sabodo alitoa ushauri huo jana
alipozungumza na JAMBO LEO katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dar es
Salaam, ambapo alisema licha ya hatua nzuri za Serikali ya Rais Magufuli
kiuchumi na kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi, wapo walioficha
mabilioni ya fedha nyumbani badala ya benki ili kukwepa kodi.
“Rais anafanya kazi nzuri, lakini ni
wengi walioficha fedha nyumbani. Watanzania wanakufa njaa, wengine wameficha
fedha. Hapo nashauri Rais abadilishe fedha hasa noti za Sh 5,000 na Sh 10,000.
Hatua hiyo itasaidia kukabili ubadhirifu unaofanywa na watu wenye nia mbaya,
lakini pia inaweza kuokoa uchumi na kufikia ndoto ya kuwa na Tanzania Mpya,”
alisema Sabodo.
Aliongeza: “Kwa maoni yangu, hatua hiyo
ya kubadilisha fedha ichukue kati ya mwezi mmoja na mmoja na nusu, watabainika
wengi walioficha fedha nyumbani na hali ya uchumi itabadilika.”
Akifafanua, Sabodo ambaye ni mzaliwa wa
Lindi, alisema India, Pakistan na Venezuela ziliwahi kukumbwa na hali kama
iliyopo sasa nchini, lakini hatua ya kubadilisha noti ilizisaidia kuimarisha
uchumi na bajeti zao.
“Watu wanaiba fedha nyingi, wanazificha
chini ya magodoro, ili kumaliza hali hiyo ni muhimu noti zikabadilishwa hali
itakayomlazimisha kila aliyeficha fedha kuzitoa, hapo wapo watakaokimbia nchi,”
alisema Sabodo huku akitaja baadhi ya watakaokimbia hatua hiyo ikichukuliwa.
Sabodo alitoa kauli hiyo wakati Rais
Magufuli ameshatoa kauli kuwataka walioficha fedha majumbani kuziacha ziingie
kwenye mzunguko huku akionya wasipofanya hivyo anaweza kuamua kuzibadili ili
wakose mahali pa kuzipeleka.
Magufuli alitoa kauli hiyo Septemba kwenye
mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi ambapo alisema watu hao wamekuwa na
utaratibu wa kutoa fedha zao benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi
walichonacho.
Wachumi
Akizungumzia
suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Profesa Damian
Gabagambi alisema: “Kuendesha uchumi hakutakiwi nguvu sana. Uchumi unajengwa kwa
imani, mtu yeyote anayeendesha uchumi anatakiwa kuijenga hiyo imani na ikuzwe.
“Chochote
kinachofanyika na kuua imani kinavuruga uchumi, ukiona watu wanaficha fedha
hilo si tatizo, ni kwamba kuna kitu ambacho ni tatizo, kuficha fedha ndio
kujihami kwao.”
Alisema
njia nzuri ya kufanya watu walioficha fedha kuzitoa, ni BoT kupunguza masharti
inayowekea benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa, jambo
ambalo litafawanya watu kutoficha fedha kwa maelezo kuwa wakipeleka fedha kwenye
benki hizo, watapata faida.
Alisema
riba inayotozwa kwenye benki inapangwa na BoT na kuitaka benki hiyo kufanya
marekebisho ili kusaidia wanaoweka fedha kwenye benki kupata faida.
“Ila
kama wana hakika fedha zimefichwa na wahusika hawawezi kuzitoa, njia pekee ni
kutishia kuchapisha, ingawa hiyo ni njia ya haraka sana. Pamoja na hayo, muhimu
ni kuhakikisha chanzo cha watu kuficha fedha kinajulikana,” alisema
Mhahidhi
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema: “Katika
uchumi ambao unakwenda vizuri na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa fedha
zinafanya kazi, suala hilo (kuficha fedha) haliwezi kujitokeza kwa maana mwenye
fedha atajua jinsi ya kuziweka.
“Katika
uchumi ambao watu wamekaa na kuhodhi fedha majumbani mwao ukitaka fedha hizo ziingie
kwenye mzunguko basi unazibadilisha. Watu watazileta kwa nguvu maana hawatakuwa
na ujanja. Ila kubadili fedha kuna sababu nyingi.”
Alisema
sababu nyingine ni kutaka kubadili fedha ili kuwa na mwonekano mpya, pamoja na
ubora wake ikiwa za awali zilikuwa zikichakaa mapema.
“Watu kukaa na fedha ndani ni kutoelewa
mifumo ya kisasa ya kibiashara, watu wanaofanya hivyo ni wanaofanya shughuli
ambazo haziko kwenye mfumo wa ulipaji kodi,” alisema.
Wapinzani
Kuhusu vyama vya upinzani, Sabodo
aliyepata kufadhili Chadema na CCM, alisema kutokana na msimamo na utendaji wa
Rais Magufuli vyama hivyo sasa vinaweza kuzipa kisogo siasa za majukwaani na
kuungana na Rais Magufuli kujenga nchi mpya kiuchumi kwani ameonesha mwelekeo
mzuri.
“Enzi za utawala wa Mkapa (Benjamin) katika
utawala wa awamu ya tatu na awamu ya pili upinzani ulikuwa muhimu kuwepo, lakini
sasa Rais Magufuli ameonesha nia njema na anafanya kazi kujenga Taifa
akipigania wanyonge jambo lililokuwa likipigiwa kelele huko nyuma.
“Ndiyo sababu ninasema hakuna haja ya
kuwa na upinzani sasa, bali wamuunge mkono Rais Magufuli tujenge Taifa,”
alisema Sabodo.
0 comments:
Post a Comment