Leonce Zimbandu
Jaji Mkuu, Othman Chande |
KATIKA kile kinachodaiwa kuwa ni
kuchoshwa na tabia ya baadhi ya mawakili, Jaji Mkuu wa Tanzania Othman Chande
amewataka mawakili 6,082 kujiepusha na ulaghai ili kuisaidia Mahakama
kusikiliza na kutoa hukumu za kesi mapema.
Chande alitoa kauli hiyo jana jijini Dar
es Salaam alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya kuwatunuku vyeti vya uwakili
mawakili 287 na kusema ulaghai hutumika kwa kusikiliza kesi muda mrefu, huku
mawakili wakiendelea kutetea.
Alisema mawakili wasikubali mawazo ya
wateja wao kwa lengo la kuchelewesha kesi kwa vile ni kinyume cha maadili,
hivyo kesi zinapaswa kuendeshwa kwa uwazi na bei inayoridhisha kwa wateja ili
haki itolewe.
“Kesi zinapocheleweshwa mahakamani imani
ya wananchi inapotea na hadhi ya Uwakili na Mahakama inashuka,” alisema.
Alisema muhimili huo ulipokea malalamiko
71 kuanzia mwaka jana hadi sasa, asilimia 45 yalibainika kuwa kumekuwa na
vitendo vya kuuzwa siri ya mteja upande mwingine wa mashtaka.
Mambo mengine yaliyobainishwa ni kushindwa
kuendesha kesi kwa viwango na baadhi ya mawakili kutoa huduma hiyo bila ya
leseni.
Mmoja wa wahitimu hao, Alex Masaba
ambaye ni Katibu wa Meya wa Ilala alisema mawakili waliopo nchini bado wachache
kutoa huduma kwa Watanzania milioni 50 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Alisema kutokana na uhaba wa mawakili
hao gharama za kesi zimekuwa juu, hivyo baadhi hutumia nafasi hiyo kufanya
biashara kwa vile wanafahamu huna njia nyingine ya kutumia.
“Namshukuru Mungu kufikia hapo nilipo, hivyo
nitashirikiana na mawakili wenzangu ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kudai haki hadi ipatikane,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju alisema mawakili wanatakiwa kuwa waadilifu na wafuate sheria ili
kuepusha malalamiko.
“Unajua wakili anapofanyakazi kwa kuzingatia
maadili hujiletea heshima, vinginevyo atapoteza heshima kwenye uwakilishi kwa
umma,” alisema.
Aidha, aliwataka mawakili hao kuendelea
kusoma ili kujiongezea elimu ilikayowasaidia katika kutekeleza majukumu yao.
0 comments:
Post a Comment