*Wasomi wasema ung’ang’anizi wa Majaliwa una kishindo
*Wasema ameshanusa kitu anatafuta
uhakika kukimaliza
Waandishi
Wetu
Kassim Majaliwa |
ANAUJUA ukweli. Ndivyo wanavyoeleza wanasiasa
na wasomi waliozungumza na gazeti hili kuhusu uamuzi wa Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, kuunda timu mpya ya kuchunguza mazingira ya kifo cha faru John,
kubainisha kuwa mnyama huyo atang’oka na vigogo wa Wizara ya Maliasili na
Utalii.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati
tofauti, walisema kitendo cha Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali kutaka kaburi la faru
huyo kufukuliwa ili kuchukuliwa vinasaba vya mwili wake na kuvilinganisha na
vya ndama wake na pembe zake wakati wa kuwasilishwa kwa taarifa ya kifo na
kuhamishwa kwake kutoka hifadhi ya Sasakwa kwenda Grumeti, kinaonesha kuwa
lazima ukweli idhihiri na hatua zichukuliwe dhidi ya ubadhirifu kama ulikuwapo.
“Waziri Mkuu ana taarifa zote na huenda
zikawa kinyume na alichoelezwa na watendaji wa mamlaka za maliasili na utalii,
akiwamo Maghembe (Profesa Jumanne-Waziri). Anachokifanya ni kujiridhisha tu na
kufuata sheria na taratibu kabla ya kuchukua hatua,” alisema Dk George
Kahangwa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(Udassa).
Desemba 6 akiwa Arusha Waziri Mkuu
Majaliwa aliagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpa
nyaraka zote zenye taarifa za kumhamisha faru Desemba 8 huku taarifa
iliyotolewa na Profesa Maghembe, ikisema mnyama huyo alihamishwa kutoka Sasakwa
na kupelekwa Grumeti, Desemba mwaka jana.
Katika maelezo yake, Waziri Maghembe
alisema uamuzi wa kumwondoa ulikuwa muhimu ili kuongeza idadi ya faru weusi na
kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Ngorongoro, na kwamba faru huyo
alikufa Agosti 18.
Kitendo cha Waziri Mkuu Majaliwa
kukabidhiwa pembe hizo na kuendelea kuwa na wasiwasi na taarifa alizopewa kama
alivyoagiza huku akitaka aoneshwe kaburi,
zimeibua wasomi hao na kubainisha kuwa haihitajiki shahada kutambua kuwa kuna
kitu kimebainika tayari.
Katika maelezo yake, Dk Kahangwa alisema
Waziri Mkuu alitumia falsafa ya kutomwamini mtu yeyote, kwamba iwapo uchunguzi
huo utatoa majibu tofauti na taarifa zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na
Utalii, lazima kuna watakaowajibika.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri mwingine
wa Chuo hicho Richard Mbunda, aliyesema “anataka kufuatilia jambo hili hadi
mwisho. Ni mfano kwa watendaji wengine wa Serikali wanaoachia mambo njiani. Sioni
lililojificha kwa wahusika wa faru huyo, ila kitendo cha Waziri Mkuu kutoridhika,
tafsiri yake ni kuwa kuna jambo limejificha. Ukweli tutaujua tu ngoja uchunguzi
ukamilike.”
Alisema sakata hilo limeibuka kipindi
ambacho nchi imekuwa na matukio mengi ya ujangili, huku akitolea mfano wa
kashfa ya kusafirishwa kwa twiga na ngedere kupitia Uwanja wa Kimataifa wa
Ndege wa Kilimanjaro (KIA), “Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuonesha
utofauti wake na awamu iliyopita.”
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk
Benson Bana alisema: “Anajua kiundani jambo hili na anachokifanya ni kuonesha kuwa yeye ni mtu anayefuata sheria. Ameunda tume,
akiamini baada ya majibu atakuwa katika nafasi muhimu ya kufanya uamuzi na
huenda tukashuhudia watu wakitumbuliwa.”
Dk Onesmo Kyauke pia wa UDSM aliungana
na Dk Bana huku akienda mbali zaidi akisema mpaka suala hilo linafika kwa
Waziri Mkuu ni wazi kuwa Waziri mwenye dhamana alishindwa kulishughulikia.
“Kama ni kweli faru huyo hajafa bali
alitoroshwa au kuuzwa, ni lazima mtu atatumbuliwa tu sambamba na watendaji
wengine. Faru wapo wachache nchini, lazima Serikali iwe macho kuhakikisha
hawapotei,” alisema.
“Unaweza ukajiuliza Maghembe alishindwa
vipi kulimaliza suala hili? Ni jambo linalofikirisha sana, lina maswali zaidi
kuliko majibu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment