Bakwata yatoa siku 7 kusalimisha mali


John Banda, DODOMA

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limetoa siku saba kwa wanaohodhi magari na pikipiki vilivyosajiliwa kwa jina la Baraza hilo kuviwasilisha kwa ajili ya uhakiki na watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo, watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mwenyekiti wa Tume ya Mufti, Shekhe Abubakari Khalid alisema Tume katika utekelezaji wa hadidu za rejea za majukumu yake, imeendelea na kazi iliyotumwa na Mufti wa Tanzania.

Shekhe Khalid alisema Tume inawataka wanaohodhi vyombo vya moto yakiwamo magari na pikipiki vilivyosajiliwa kwa jina la Bakwata  mkoa wa Dar es Salaam, waviwasilishe vihakikiwe katika ofisi za Bakwata makao makuu barabara ya Kinondoni, Dar es Salaam, kuanzia jana.

“Walio mikoani waviwasilishe katika ofisi za Bakwata za mikoa husika, pia makatibu wa mikoa watekeleze ndani ya muda huo, maagizo waliyopewa kuhusu kadhia hiyo,” alisema.

Alisema baada ya siku saba kupita, Bakwata kwa kushirikiana na mamlaka husika, itaendesha msako mkali na kuchukua hatua za kisheria kwa ambao hawatatekeleza agizo hilo.

Alisema Tume inashukuru wanaoendelea kutoa ushirikiano na kuipa taarifa muhimu kuhusu mali zinazomilikiwa kinyume cha sheria na kuwataka waendelee kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa ambaye ni mjumbe wa Tume hiyo, Shekhe Khamis Mataka alisema kuna suala la taasisi za dini kupata misamaha kwenye kodi, hivyo uhakiki huo una lengo la kupata idadi ya magari na pikipiki yaliyopewa msamaha kwa nchi nzima.

“Uhakiki huo pia utasaidia kujua idadi ya magari yaliyopo na hali zao kwani kuna mengine yamekwisha na hayatumiki tenam na ni vizuri kufanya uhakiki,” alisema.

Pia alisema uhakiki huo baadaye utahamia kwenye mali zingine za Baraza hilo zikiwamo nyumba na viwanja.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo