Joyce Anael, Same
MOTO mkubwa umezuka katika maeneo ya Ofisi
ya Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro na kusababisha hasara kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na
baadhi ya mashuhuda, moto huo ulianza majira ya saa moja na nusu usiku Jumamosi
iliyopita ukianzia katika ofisi za usajili wa vyeti vya vizazi na vifo Rita.
Walisema moto huo uliziteketeza kabisa
ofisi za Uhamiaji, Rita, ofisi ya mshauri wa mgambo, stoo na masjala.
“Umeme ulikuwa umekatika na uliporudi,
ghafla niliona moto mkubwa ukitokea kwenye ofisi za Rita na kuenea kwenye ofisi
zingine na ndipo nikaanza kufanya mawasiliano ambayo yalipelekea wananchi
kujitokeza kwa wingi kutoa msaada”, alisema mlinzi aliyekuwa zamu siku ya
tukio, Kighono Saidi.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Sitaki
Senyamule amesema athari kubwa iliyotokea ni kutokana na ukosefu wa huduma ya
zimamoto wilayani humo.
“Tulitoa taarifa ya moto huu mapema,
lakini hakuna huduma ya zimamoto katika wilaya yetu wala wilaya jirani ya
Mwanga na hili limechangia athari kubwa,” alisema.
Alisema ili kupata ufumbuzi wa haraka
ilibidi gari la zimamoto litokee mjini Moshi ambako ni umbali wa zaidi ya
kilomita 100 kutoka wilayani Same na kwamba lilichukua takribani saa mbili
kufika mjini humo na kukuta athari kubwa ishatokea.
Rosemary aliendelea kusema kuwa kuna
haja ya kuwepo kwa huduma hizo kila wilaya ili kuepuka athari za namna hiyo
zisitokee tena wakati mwingine.
Aliwapongeza wananchi waliojitokeza
kuuzima moto huo ambao hata, hivyo alisema ulikuwa ukikua kwa kasi kutokana na
mazingira ya upepo mkali yaliyoko katika wilaya hiyo.
Katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro,
Aisha Amour aliyefika eneo la tukio na kujionea hali ilivyo, alisema kuna haja
ya miundombinu ya umeme kuangaliwa upya katika majengo yote ya serikali mkoani humo.
Aidha alitoa muda wa siku mbili kwa
TEMESA, kwa ushirikiano na TBA na idara ya zimamoto kumpa taarifa ya madhara
yaliyotokana na moto huo.
0 comments:
Post a Comment