*Naibu wake atoa mwito wananchi
wajikinge
Waandishi Wetu
WAKATI Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akisema ugonjwa wa zika
haujaingia, nchini, Naibu wake Dk Khamis Kigwangalla ametaka wananchi wajikinge
nao kama wafanyavyo kwa malaria.
Hata hivyo, Mwalimu aliwataka wananchi
kuondoa hofu ya ugonjwa huo kwa vile haujathibishwa kuwapo nchini.
Waziri katika taarifa yake jana, alisema
utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na
matokeo yake kutangazwa juzi, ulihusu kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha magonjwa
ya zika na chikungunya.
Mwalimu alisema hayo alipokuwa akitoa
ufafanuzi wa taarifa ya utafiti ya zika nchini kwa waandishi wa habari Dar es
Salaam.
Alisema utafiti uliofanywa na NMRI
kitaifa ni hatua za awali za kuangalia ubora wa kipimo, hivyo matokeo hayo
yanapaswa kuchunguzwa kwa kina kupitia vipimo vilivyothibishwa na Shirika la
Afya Duniani (WHO).
“Wizara yangu itashirikiana na taasisi
za ndani na nje ya nchi, kuendeleza utafiti na ufuatiliaji wa kitaalamu, ili
kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini,” alisema.
Alisema sekta ya afya ina utaratibu wa kutoa
taarifa ya magonjwa ya kuambukiza ambayo ni hatari, ikiwamo zika, ebola na
mengineyo, hivyo mikakati ya ufuatiliaji wa zika imeandaliwa na taarifa
itatolewa.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwele
Malecela alisema taasisi hiyo ilifanya utafiti wa ubora wa kipimo kipya, ili
kujiridhisha kama kina uwezo wa kupima virusi vya zika.
“Taarifa yangu ilitoa matokeo ya virusi
vya zika vinavyoweza kusababisha watoto kuzaliwa na kichwa kidogo,
haikumaanisha kuwepo kwa ugonjwa huo, tunafahamu Wizara ndiyo yenye dhamana ya
kutangaza,” alisema.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa
Mohammed Bakari alisema wataalamu wataendelea kuzifanyia uchunguzi taarifa za
NIMR ili kujiridhisha.
“Wataalamu wakikamilisha uchunguzi wa
taarifa, utaratibu utaandaliwa baada ya kujiridhisha, lakini hivi sasa Mamlaka
haijajiridhisha kwa vile ni taarifa za awali,” alisema.
Dk Kingwangwala alitaka wananchi waondoe
hofu, kwani hakuna tofauti ya kujikinga zika na malaria.
“Tunapaswa kutumia vyandarua kuzuia mbu
na kutunza mazingira, huku Serikali ikiendelea kuchunguza taarifa za awali za
NIMR, ili kutoa taarifa rasmi,” alisema.
Juzi Dk Mwele alikutana na waandishi wa habari kueleza
ripoti ya utafiti wao ikionesha zika kuwapo nchini na kuendelea na utafiti
kujua ukubwa wa tatizo.
Utafiti huo ulifanyika kati ya mwaka jana na mwaka huu
katika mikoa minane na jumla ya sampuli 533 za damu zilipimwa na kati yao,
watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo.
Baada ya utafiti walibaini kuwa asilimia 43.8 ya watoto
wachanga waliambukizwa virusi vya zika.
Mikoa iliyofanyiwa utafiti ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga,
Geita, Kigoma, Tabora, Singida na Morogoro, na bado taasisi hiyo na Chuo Kikuu
cha Bugando, Mwanza wanaendelea na utafiti ili kujua ukubwa wa tatizo hilo kwenye
mikoa hiyo.
Dk Mwele alitoa taarifa hiyo wakati akielezea mafanikio
ya taasisi yake kwa mwaka mmoja na kusema kati ya watu 533 waliopimwa, 83 (asilimia
15.6) waligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya zika na hivyo kupewa
matibabu haraka.
“Kwa wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu,
asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya zika na hadi sasa bado
tunaendelea na utafiti kubaini ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za
haraka,” alisema Dk Mwele.
Leonce
Zimbandu na Jemah Makamba
0 comments:
Post a Comment