Abraham Ntambara
Jaji Steven Bwana |
TUME ya Utumishi wa Umma nchini imezitaka mamlaka za
ajira, watumishi wa umma na waajiri kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na
nidhamu wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana Dar es
Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Steven Bwana ilisema Tume ilifanya
mkutano wa wiki mbili ikapokea na kujadili taarifa za ukaguzi wa rasilimaliwatu
katika taasisi kadhaa za umma.
Alisema miongoni mwa taasisi zilizojadiliwa ni Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu Dodoma (CDA), wakala
wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Manispaa ya Ilala na Manispaa ya Kinondoni na
kubaini ukiukwaji wa taratibu.
“Katika kaguzi hizo na kushughulikia rufaa ilibainika
kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu miongoni mwa watumishi wa
umma, waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu,” alisema Jaji Bwana.
Alisema baadhi ya viashiria vikubwa vya udhaifu
vilivyojitokeza ni pamoja na tabia mbaya kwa baadhi ya watumishi wa umma iliyosababisha
kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria na kinidhamu.
Viashiria vingine alisema ni mamlaka za nidhamu kushindwa
kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria watumishi wenye utendaji mbovu, huku
baadhi ya mamlaka zikishindwa kuunda kamati za uchunguzi au kutotumia taarifa
za uchunguzi wa awali kama zilivyowasilishwa kwao.
Aliongeza kuwa vingine ni kufungua mashauri ya nidhamu na
kukaa muda mrefu bila kuyahitimisha huku pia wakibaini upungufu kwenye uandaaji
na uendeshaji mchakato wa mashauri.
Jaji Bwana alisema walibaini upandishwaji vyeo watumishi
bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ambapo Tume ilisisitiza watumishi wa
umma, waajiri na mamlaka za nidhamu kuzielewa na kuzizingatia wakati wote.
Aliwataka viongozi wa halmashauri waelewe, wazingatie na
waelimishe watendaji wa vijiji na kata kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa sheria,
kanuni na taratibu wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Alisema kwenye mkutano huo wa wiki mbili Tume
ilishughulikia na kutoa uamuzi wa rufaa 42 na malalamiko mawili ambapo rufaa 31
zilikataliwa na nane kukubaliwa bila masharti huku tatu zikikubaliwa kwa
masharti kwa kutakiwa kuanza upya kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
0 comments:
Post a Comment