Abraham Ntambara
KAMPUNI ya Mabasi Yaendayo Haraka
(UDA-RT) imekiri changamoto ya chenji ya Sh 50 na kusema ufumbuzi wa tatizo
hilo ni kutumia kadi za elektroniki.
Akizungumza na JAMBO LEO jana Dar es
Salaam Ofisa Uhusiano wa Udart, Deus Buganywa alisema mfumo ulivyo na
ulivyoandaliwa unatakiwa kutumia kadi kwa asilimia 90.
“Kwa maana kwamba matumizi ya tiketi
yawe kwa asilimia 10 au chini ya asilimia 10,” alisema Buganywa.
Alisema kutumia kadi kutaondoa usumbufu
wa watu kukaa kwenye foleni wakisubiri kununua tiketi ambapo alibainisha kuwa
pia itakuwa imesaidia kutatua kero ya chenji.
Aliongeza kuwa mtu anapokuwa na kadi
huitumia kwa matumizi binafsi kwa sababu inampa fursa ya kulipia nauli hata kwa
njia ya simu na hivyo kumwepusha adha hiyo.
Buganywa alisema teknolojia ya kadi
lengo mojawapo ni kuondoa kero ya chenji.
Alisema pamoja na tatizo hilo wamejitahidi
kukabiliana nalo kwa kutafuta chenji kutoka benki lakini pamoja na juhudi hizo
bado tatizo liko pale pale kwa kuwa wanapata chache hivyo hazitoshelezi
mahitaji.
Alieleza kwamba wamekuwa wakijitahidi kuzitafuta
lakini zinapopatikana zinakuwa chache akibainisha kuwa ili kukabiliana zaidi na
tatizo hilo wameanzisha dirisha maalumu la chenji.
Dirisha hilo kazi yake ni kukusanya
fedha za mfumo wa chenji zinazoletwa na abiria, ili kusaidia wanaohitaji chenji.
0 comments:
Post a Comment