Sharifa Marira
Makao Makuu ya CCM Dodoma |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeanza
uhakiki wa mali zake ambapo hadi sasa kimehakiki kata 40 huku kikitarajia
kupitia kata 102.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa, Juma Gadafi alisema lengo la uhakiki huo ni
kutekeleza maagizo ya chama na kuboresha utendaji.
‘’Tunaendelea na uhakiki wa mali za chama, tumeshapita
kata 40 lengo ni kata zote 102 ambazo tuna imani hivi karibuni tutakamilisha
uhakiki ili kuboresha utendaji wa chama,’’ alisema Gadafi.
Katika hatua nyingine, chama kimempitisha Tausi Milanzi
kuwa mgombea udiwani kata ya Kijichi na kwamba kinatarajia kupata ushindi wa
kishindo kutokana na sera za CCM kutetea wanyonge na mgombea wake anatarajiwa
kuchukua fomu kesho.
Alisema Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya
utekelezaji wa Ilani ya chama, hivyo hapana shaka wananchi kuunga mkono ushindi
wa chama hicho kata ya Kijichi, ili kuendeleza utekelezaji wa ahadi zake.
“Kamati ya Siasa ya Mkoa ilipokea majina 12 ya wagombea
udiwani wa kata ya Kijichi waliotokana na kura za maoni kwa kuzingatia kanuni
na sheria, tumemteua Milanzi kupeperusha bendera na tuna imani atakwenda
kusimamia utekelezaji wa Ilani,’’ alisema Gadafi.
Akizungumzia uteuzi wa nafasi ndani ya CCM uliofanywa hivi
karibuni na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli alisema umezingatia mahitaji ya
chama hicho, katika kupigania maslahi ya wananchi.
Alisema kutokana na safu ya uongozi iliyopo inawataka wahujumu
maendeleo kwa makusudi ikiwemo wanaokwepa kulipa kodi na kuacha mara moja kwa kuwa
hawatakuwa na pa kukimbilia.
“CCM iliyopo ni ya kisayansi na imefanya mkutano wake wa
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa siku moja lakini kulitoka na
uamuzi mzito wenye maslahi makubwa kwa chama na kwa sasa tunasubiri Mkutano
Mkuu upitishe maazimio hayo na kuanza utekelezaji wake,” alisema.
Alisema CCM Mkoa itahakikisha inashirikiana na kufanya kazi
na viongozi walioteuliwa ili kuleta ufanisi.
0 comments:
Post a Comment