Mwandishi Wetu, Arusha
Kassim Majaliwa |
SIKU 10 baada ya kupokea taarifa
inayoeleza utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya
Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko Hifadhi ya Grumeti,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu kuchunguza utaratibu
huo, ikiwa ni pamoja na kutafuta kaburi alikozikwa.
Majaliwa amesema timu hiyo ya wataalamu
tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi la faru huyo
aliyeripotiwa kufa, kuchukua vinasaba vya masalia yake na kisha kwenda Hifadhi
ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kuvilinganisha na pembe
ambazo alipelekewa kama ushahidi wa kifo cha faru huyo.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu imefufua upya
sakata hilo baada ya Desemba 9 mwaka huu kupokea taarifa ya kuhamishwa kwa faru
huyo ambaye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema
alihamishwa kwa sababu ya kupunguza tatizo la 'Inbreeding' ndani ya Hifadhi ya
Ngorongoro.
Katika maelezo yake wakati akisoma
taarifa hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Taifa ya kuwalinda tembo na faru,
Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kuzorota na
alikufa Agosti 18 mwaka huu.
Sakata hilo liliibuka Desemba 6 mwaka
huu, ambapo akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha
faru maarufu kwa jina la 'John' kutoka kwenye hifadhi hiyo, ndani ya siku
mbili.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za
makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza
na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji, ikiwa ni
sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Kitendo cha jana Waziri Mkuu kuibua tena
suala hilo ni wazi kuwa kutawapa wakati mgumu watendaji wa mamlaka zilizohusika
kumhamisha, sambamba na kutoa taarifa za awali, ikiwemo pembe za faru huyo
kuthibitisha kifo chake.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya
iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa
huduma kwa wananchi Majaliwa alisema, "Tume niliyounda kwa ajili ya
uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet Serengeti kujiridhisha kama kuna
kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda
Creter na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja.
Lengo ni kutaka kubaini kama pembe
iliyowasilishwa kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John.”
"Wakati faru John akiwa V I P
Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza
akabaini faru huyo hakuwa na ugonjwa wowote. Daktari alimpima tena kwa mara ya
pili taarifa zikasema tena si mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani."
Waziri Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo
kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali
imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini. "Ni
lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa Taifa."
Awali, wakati akipotea taarifa ya faru
huo Waziri Majaliwa alisema itafanyiwa kazi jambo ambalo linaashiria kuwa kazi
hiyo imeshaanza kufanyika kutokana na agizo alilolitoa jana.
Alichokisema Maghembe
Wakati akiwasilisha taarifa hiyo Waziri
Maghembe alisema, hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa
alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya
kreta.
“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya
kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John
ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo
la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri
Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa
tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya
Kuwalinda Tembo na Faru.
Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu
wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu
wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya
Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa
Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na
uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
0 comments:
Post a Comment