Abraham Ntambara
Isaya Mwita |
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya
Mwita, anatarajia wiki hii kufanya mazungumzo na kampuni zilizopewa mamlaka ya
kusimamia na kudhibiti maegesho mabaya ya magari kwa kuwa wanatumia fursa hiyo kama
kitega uchumi, huku wakisababisha kero kwa wananchi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa
malalamiko kutoka kwa wakazi wa jiji dhidi ya vitendo vya kampuni hizo kukamata
hovyo magari hayo kwa kisingizio cha kuegeshwa mahali pasiporuhusiwa na kuwatoza
faini wamiliki.
Akizungumza na JAMBO LEO jana alisema
kuna kampuni mbili ambazo zilipewa mamlaka hayo na kubainisha kuwa watendaji
wake wamekuwa wakikamata magari na kutoza faini kinyume na utaratibu.
“Tulikuta kuna sheria ndogo za jiji
zenye lengo la kuzuia uegeshaji hovyo wa magari, hivyo watendaji wa kampuni
hizo wanatekeleza kazi hiyo vibaya. Wanataka kufanya jiji hili liwe shamba la
bibi,” alisema Mwita.
Mwita alisema magari ambayo yanatakiwa
kukamatwa na kutozwa faini tena iliyowekwa kisheria ni yale ambayo yameegeshwa
pembeni ya barabara, lakini watendaji wake wamekuwa wakikamata hata ambazo
hazina makosa na kuwatoza faini tena kiwango kikubwa tofauti na kiwango
kinachotakiwa.
Aidha aliongeza kuwa yeye alichaguliwa
ili kuhakikisha anatatua changamoto za wakazi wa jiji la Dar es Salaam, hivyo
hana budi kuwatetea na kuwaondolea changamoto hizo.
Meya huyo alibainisha kuwa hadi sasa
kuna mkataba mwingine wenye lengo la kufanya shughuli hiyo katika halmashauri
ya Manispaa ya Temeke ambao unatakiwa ausani, lakini amekataa kuusaini mpaka
baadhi ya masharti yaliyomo yaondolewe.
Pia, alisema hata kwa manispaa nyingine
za Ilala na Kinondoni mikataba ya namna hiyo haitasainiwa kama itakuwa na
masharti ambayo yatakuwa kero kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment