Mwandishi Wetu
RAIS John Magufuli, amewaapisha viongozi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
na majaji wa Mahakama ya Rufani aliowateua juzi.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
Ikulu, Gerson Msigwa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa hafla
ya kuwaapisha viongozi hao, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Anjellah Kairuki, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju na viongozi wengine.
Walioapishwa ni Jaji Semistocles Kaijage
kuwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, kuwa Makamu Mwenyekiti
wa NEC na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Harold Nsekela kuwa Kamishna wa
Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Viongozi hao watashika
nyadhifa hizo kwa miaka mitano.
Majaji walioapishwa kwa ajili ya
Mahakama ya Rufani, ni Jaji Rehema Mkuye; Jaji Sivangilwa Mwangesi, Jaji Gerald
Ndika na Jaji Jackobs Mwambegele.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana
na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini, Yesamin Eralp ambapo
viongozi hao walizungumzia uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki, hususan katika
masuala ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.
Aidha, Rais Magufuli na mkewe Mama
Janeth, walimtembelea na kumpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kumpa pole ya kifo cha dada yake
Efrazia Pengo (79), aliyefariki dunia juzi katika kijiji cha Mwazye, wilaya ya
Sumbawanga, Rukwa.
Rais Magufuli na Mama Janeth walimtembelea
Kardinali Pengo katika makazi yake Kurasini, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment