Charity James
WACHEZAJI wa Tanzania wameamka sasa,
wamekuwa wakitoka kwa wingi nchini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta
timu zenye malisho mazuri zaidi ya timu za hapa nyumbani.
Idadi hiyo ya wachezaji kuondoka nchini
kwenda nje imekuwa kubwa tofauti na miaka mingine ambayo kulikuwa hakuna
mchezaji anayecheza ligi katika nchi jirani.
Moja ya kitu ambacho tumekikosa kwa wakati
huu ni kupata kundi kubwa la makocha ambao watakwenda kufundisha soka nje ya
nchi, lakini kwa mwenendo uliopo sasa, Tanzania itakuwa na kundi la makocha
ambao watakuwa wakifundisha soka nje ya nchi.
Nahodha wa kikosi cha Taifa Stars na
mshambuliaji wa klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ni baadhi ya
wachezaji wa Tanzania ambao hivi sasa wanaipeperusha vyema bendera ya nchi na
kila mmoja anafahamu kuna nchi inaitwa Tanzania, anakotoka mshambuliaji Samatta.
Samatta ni kioo nje ya mipaka ya Tanzania
baada ya hivi karibuni kujiunga na klabu ya Konibklijke Racing Club Genk (KRC),
ya Ubelgiji akitokea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidomakrasi ya Congo (DRC).
Kwa kutambua mchango wa Samatta na baadhi
ya wachezaji wengine wanaocheza nje ya nchi, hii ni orodha yao wanaopeperusha
bendera ya nchi.
Samatta
Ndiyo nahodha wa Taifa Stars, akichukua
kitambaa hicho kutoka kwa mkongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Nyota huyo anasimama kama mchezaji mwenye
mafanikio, ukilinganisha na nyota wengine nchini, kutokana na kufanya vema katika
soka.
Samatta alianzia maisha yake ya soka katika
klabu ya Kimbangulile FC, kisha Mbagala Market ambayo sasa ni African Lyon na
baadaye Simba, amekuwa balozi wa wachezaji wa Tanzania nje ya nchi.
Mafanikio ya Samatta akiwa na TP Mazembe,
yalimfanya aingie kwenye historia ya timu hiyo kama miongoni mwa wachezaji bora
waliowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa klabu hiyo ya Lubumbashi inayomilikiwa
na Moise Katumbi.
Mrisho Ngassa
Nyota huyo anayecheza soka la kulipwa nchini
Oman kwenye klabu ya Fanja ya nchini humo, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya
Free State Stars ya Afrika Kusini, ni miongoni mwa wachezaji bora nchini kwa
miaka ya hivi karibuni ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye klabu na timu ya
taifa.
Ngassa aliyechipukia kisoka katika klabu ya
Channel ya kwao Mwanza, kabla ya kusajiliwa Kagera Sugar na baadaye Yanga ni
winga mahiri ambaye ana uwezo wa kufunga mabao.
Ubora wa Ngassa umemfanya kuwa miongoni mwa
wachezaji waliowahi kuzichezea timu kubwa nchini za Yanga, Simba na Azam.
Nyota huyo aliwahi kufanya majaribio katika
klabu ya West Ham ya England na Seattle Sounders ya Marekani, alishindwa kuishawishi kumsajili, huku mwaka 2012, akikataa kwenda
kujiunga na El Merreikh ya Sudan, iliyokuwa ikimtaka bila kufanya majaribio.
Elius Maguli
Ni mshambuliaji wa zamani wa Simba na Stand
United, ambaye kwasasa anakipiga katika timu ya, Dhofar SC ya Oman, amekuwa na
mafanikio makubwa katika kikosi chake kipya kutokana na kupata nafasi ya
kucheza kikosi cha kwanza.
Ni mchezaji ambaye ameweza kujipatia
mafanikio makubwa katika michezo ya ndani akiwa katika timu zake na kufanikiwa
kujipatia nafasi ya kucheza katika kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars'.
Emily Mgeta
Mgeta ni kati ya wachezaji waliokuwa
wakiunda timu ya vijana ya Simba B, iliyokuwa na wakali wengine Said Ndemla,
Rashid Mkoko na Ibrahim Ajib.
Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya ulinzi
wa kushoto hivi sasa anacheza soka la kubwa katika klabu ya Neckasulm,
inayoshiriki ligi daraja la tano nchini ya Ujerumani.
Mgeta alivyokuwa nchini alizitumikia timu
za Simba B na baadaye kupandishwa A, Villa Squad na Polisi Morogoro ambayo hadi
anaondoka kwenda Ujerumani alitokea timu hiyo.
Nyota huyo amezoea maisha ya Ujerumani
baada ya kuwa na mtoto nchini humo ambaye amezaa na mmoja ya raia wa nchi hiyo.
Thomas Ulimwengu ‘Buffalo’
Pacha wa Samatta katika kikosi cha Stars.
Nyota huyo amekataa kusaini mkataba mpya wa kuichezea TP Mazembe, msimu
uliopita alikuwa na Samatta na kutengeneza muungano mzuri ulioipa mafanikio
makubwa klabu hiyo.
0 comments:
Post a Comment