Hussein Ndubikile
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu Nchini (HESLB) imesema kuwa itapita nyumba kwa nyumba, nyumba za ibada na
kwenye sherehe kubaini na kuwakamata wadaiwa sugu wa mikopo ambao hawajawasilisha
taarifa zao na kurejesha mikopo hadi sasa.
Aidha, Bodi hiyo tangu ilipotoa notisi
ya mwezi mmoja imekusanya Sh bilioni 140 kati ya Sh bilioni 300 ilizokuwa ikidai
wanufaika wa mikopo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alisema
tangu notisi itolewe kwa wadaiwa hao na kuongeza wiki mbili, mwitiko umekuwa
mkubwa na kuwezesha kiasi kikubwa cha fedha kukusanywa huku ikisisitiza kulazimika
kufanya operesheni hiyo kubaini wadaiwa wanaokwepa kurejesha fedha hizo.
"Wiki tatu zilizopita tulitoa ofa
kwa wadaiwa, tulianza na wiki nne tukaongeza nyingine mbili, wengi
waliojitokeza walirudisha kiasi kikubwa cha mikopo, tunaomba ambao hawajamaliza
walipe baada ya muda wa nyongeza wa kulipa, hiari ikimalizika tutapita nyumba
hadi nyumba, nyumba za ibada na kwenye sherehe, naamini tutawapata
wadaiwa," alisema.
Alisema katika kuhakikisha inatia
nguvuni wadaiwa, Bodi itashirikiana na wadau wakiwamo watumishi wake, majirani
na idara na taasisi za Serikali kupata
taarifa zao.
Badru alisema baada ya kumalizika muda
wa kurejesha kwa hiari, kuanzia Januari mosi bodi itachapisha majina na sura za
wadaiwa sugu ili umma uwaone na kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwamo
kuwakamata na kulazimika kulipa gharama za kuwatafuta.
Alisisitiza kuwa wadaiwa wa mikopo 42,700 kati ya 142,000 walijitokeza
kulipa fedha hizo tangu Bodi itoe notisi ya mwezi mmoja na kwamba wanufaika walio kwenye mfumo rasmi
wa ajira watakatwa asilimia 15 na wasio kwenye mfumo huo watakatwa asilimia 10
ya kipato chao.
Alisema kiwango cha wastani wa makusanyo
ya mwezi kimeongezeka kutoka Sh bilioni 2 kwa Januari na Juni Sh bilioni 4 huku
Novemba yakiongezeka hadi Sh bilioni 8.
Aliongeza kuwa muda wa kurejesha mikopo
kwa wanufaika waliomaliza elimu ya juu uliongezwa kutoka mwaka mmoja hadi
miwili baada ya kuhitimu.
Pia alisema Bodi imeunda kikosikazi
kitakachokuwa na jukumu la kuwazungukia waajiri ambao hawajaingiza makato ya
mikopo ya miaka ya nyuma na wanaoingiza kiasi pungufu cha fedha.
Alifafanua kuwa waajiri walipewa siku 14
kuhakikisha wanawasilisha fedha hizo na taarifa za waajiri walionufaika na
mikopo, la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mwanasheria wa Bodi hiyo, Luhano Lupogo
alisema makato hayo yalianza kutumika Novemba 18 na kwamba waajiri
watakaoshindwa kuwajibika watalipa faini isiyopungua makato hayo au kifungo cha
miezi 36 jela.
0 comments:
Post a Comment