Salha Mohamed
Dk Harrison Mwakyembe |
SERIKALI imesema itajadili kushusha
kiwango cha fedha za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye Mahakama ya Mafisadi
ili kukomesha vitendo vya rushwa.
Pia Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam inakusudia
kujenga mahakama za mwanzo 20 mwakani kwenye wilaya zote jijini humo lengo likiwa
ni kupunguza kesi zinazokaa muda mrefu.
Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya
kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda, Waziri wa Katiba na
Sheria, Harrison Mwakyembe alisema Wizara ilianza mapema kuhakikisha inafanya
mabadiliko ya sheria ya kuunda Divesheni Maalumu ya Mahakama ya Mafisadi.
“Waandishi waliuliza tangu Julai hadi
sasa kungekuwa na kesi nyingi, lakini kuna kesi moja…tumekuja kubaini kwamba
uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,” alisema.
Alisema kwa sasa waliozoea kupora
mabilioni ya fedha wamerudi nyuma ambapo wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh
bilioni moja.
“Sisi Serikali tukiona wizi sasa umepungua
na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500 na 700 tumeanza kujadiliana
kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha, ili kukomesha udokozi,
ubadhirifu, wizi wa fedha au mali ya umma,” alisema.
Mwakyembe alisema katika mwaka mmoja,
wamepitisha sheria ya kulinda watoa taarifa na mashahidi, ili kuiwezesha
divisheni ya hiyo na wapelelezi kupata ushahidi wa kutosha.
Alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo,
Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya
kwenda mahakamani kuwa ni mzuri.
“Sisi tayari tumepeleka Muswada wa
Msaada wa Kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao
ndio wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda,” alisema.
Alisema kuanza kwa sheria hiyo
kuitafanya kuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900. ”Naupongeza
mkoa kuwa wa kwanza vijana kuanza kazi na baada ya muda mtakuwa walimu wa
kwanza kwa hili suala,” alisema.
Alisema bado kuna tatizo wanalopaswa kuliangalia
kwa pamoja ambalo ni nidhamu na maadili ya watendaji ndani ya Mahakama.
Makonda alisema walijadili utoaji na
upatikanaji wa haki kwa wakati, kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na
kuchelewa kupata haki zao.
0 comments:
Post a Comment