Sharifa Marira
Maxence Melo |
MWANASHERIA Mkuu wa Chadema,Tundu Lissu,
amesema wameandaa timu ya kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania leo asubuhi kuiomba
iagize mmiliki wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo, afikishwe mahakamani.
Akizungumza na JAMBOLEO jana, Lissu
alisema watakwenda kumwomba Jaji Mkuu, Othman Chande, atoe amri kwa Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Simon Sirro wamfikishe Melo mahakamani na kueleza kosa lake.
‘’Tunataka kuona Melo akifikishwa mahakamani
na tuelezwe anashitakiwa kwa kosa gani kwani kumfungia mahabusu na kudai
mnamfundisha adabu si njia nzuri kisheria,’’ alisema Lissu.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa sharia, mtu
anaposhikiliwa na Polisi hutakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 na
kwamba kinachofanyika sasa ni uvunjifu wa sheria ambao haukubaliki.
Alisema pamoja na mambo mengine, watamwomba
pia Jaji Mkuu awaulize viongozi hao, sababu ya kukamata mtu kwa siku tatu bila
kumfikisha mahakamani na waeleze sheria hiyo wameitoa wapi.
‘’Hata kama jalada la Melo liko kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hapaswi kufungwa na polisi bila kufikishwa
mahakamani, alipaswa kushitakiwa ndani ya saa 24 ili ajue anashitakiwa kwa kosa
gani na si kumfunga,‘’ alisema Lissu.
Alisema viongozi wanapaswa kutii sheria,
ili wananchi wa kawaida waige kutoka kwao, tofauti na yanayofanyika sasa ya
kukanyaga sheria kila siku tena kwa makusudi.
0 comments:
Post a Comment