Moses Ng’wat, Mbeya
MAPYA yameibuka sakata la kukwama
kufungwa kwa ndoa ya Samwel Mwakalobo na Ginen Mgaya, baada ya kubainika kuwa moja
ya sababu ni Bibi harusi mtarajiwa kuendeleza uhusiano na mzazi mwenzake.
Habari zimedai kuwa kabla ya mpango wa
kufunga ndoa hiyo, Mgaya tayari alishapata mtoto kabla hajaolewa, na Bwana
harusi kubaini dakika za mwisho kuwa wawili hao walikuwa bado wana uhusiano wa
karibu.
Habari hizo za ndani kutoka familia ya Bibi
harusi, zilidai kuwa kilichofanya Bwana harusi amtelekeze Bibi harusi ni
wasiwasi aliokuwa nao juu ya uhakika wa ujauzito wa mkewe huyo mtarajiwa, kuwa
ni wake kweli au wa mpenzi wake huyo wa zamani.
“Hofu hiyo ilijengeka kutokana na taarifa
alizoziamini Bwana harusi kuwa Bibi harusi anaendeleza uhusiano na mzazi mwenziwe.
Ni hofu tu ambayo angeifanyia kazi na angegundua kuwa haina ukweli wowote,” kilidai
chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kudai: “Unajua
muda mwingine binadamu tunahitaji kufanya uamuzi kwa kutafakari … maana shemeji
yetu (Bwana harusi) alipigiwa simu na mzazi mwenza wa Bibi harusi na kuelezwa
maneno ya ‘shombo’ na yeye bila kufanyia utafiti, akaamua kususa harusi.”
Wakati taarifa hizo zikibainisha hayo, familia
ya Bwana harusi imeendelea kufanya jitihada za kuhakikisha suala hilo
linamalizika kistaarabu.
Anayeelezwa kufuatilia suala hilo kwa
karibuni ni kaka yake, ambaye hadi jana jitihada za kumtafuta mdogo wake zilikuwa
zimeshindikana kutokana na kutopokea simu yake ya mkononi mara zote.
“Anayeongoza familia ya Bwana harusi ni
kaka yake. Inasemekana pia kuwa wawili hao waliingia kwenye mgogoro dakika za
mwisho kabla ya harusi na ndiyo maana baada ya kutoweka hataki hata kupokea
simu,” kilieleza chanzo kingine.
Awali, mpambe wa Bibi harusi alieleza
kuwa siku mbili kabla ya harusi hiyo, Bwana harusi alikuwa kwenye migogoro ya
kifamilia na ndugu zake kuhusu fedha za sherehe na mpaka siku ya sherehe, suala
hilo walikuwa hawajalitatua.
“Lakini tunashukuru kaka yake ni
mstaarabu, aliamua kuonesha upendo kwa mdogo wake na amekuwa akilifuatilia
suala hilo ili limalizike kwa amani, lakini mdogo mtu hapatikani,” alisema
mpambe huyo.
Alisema jitihada za Bibi harusi kumtafuta
Bwana harusi hazijazaa matunda, kwani hadi juzi alikuwa hapatikani hata
nyumbani kwake, ingawa redio ilikuwa inasikika ndani ya chumba hicho
kilichofungwa kufuli kwa nje.
Simu ya Bwana harusi ilikuwa ikiita muda
mwingi bila kupokewa, lakini hatua zingine zilidai kuwa Bwana huyo ambaye ni
mfanyabiashara kwenye kituo cha mabasi yaendayo Chunya eneo la Isanga jijini
Mbeya hajafungua duka lake.
Jitihada za kumpata Bwana harusi azungumzie
suala hilo ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mwingi bila
kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, alijibu kifupi: “Siko kwenye
mazingira ya kuzungumzia suala hilo.”
Alipozidi kubembelezwa ili azungumze, alijibu
kwa kifupi kupitia ujumbe wa simu: “Fungua data nimekutumia kwenye WhatsApp.” Hata
hivyo ujumbe huo nao haukuonekana.
Bibi harusi naye alionekana kutotaka
kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila
kupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu, ingawa muda mwingi simu
yake iliashiria kuwa akizingumza na watu wengine.
0 comments:
Post a Comment