Mwandishi Wetu, Tabora
Edward Lowassa |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward
Lowassa, ametaka vijana wa chama hicho kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia
aliodai unafanywa na watawala.
Alisema hayo juzi alipokutana na vijana
wa chama hicho ambao ni wanavyuo (CHASO) wa vyuo vikuu mkoani hapa.
Lowassa ambaye yuko hapa kwa ziara ya
kuimarisha chama, aliwataka vijana hao kuwa na ujasiri wa kukabiliana na
ukandamizaji wa demokrasia kwani vijana duniani ndio chachu ya mabadiliko.
“Nimekuja Tabora kuwashukuru kwa kura
nyingi mlizonipigia na hamasa kubwa mliyoionesha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
jana. Katika uchaguzi ule tulishinda, lakini ushindi mkubwa zaidi ni
tulipofanikiwa kuvumilia na kuweka maslahi ya watoto, wazee na mama zetu mbele,"
alisema na kuongeza:
"Amani ni tunu muhimu sana kwa
mustakabali wa Taifa kuliko kitu kingine chochote. Msikate tamaa, tumejipanga
vema kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2020 na
hatutadhulumiwa tena haki yetu, kama ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani,
alisema Jambo Kuu na la msingi ambalo wana Chadema wanatakiwa kuwa nalo sasa
katika chama ni umoja na mshikamano kati
yao.
"Umuhimu wa umoja na mshikamano
ndani ya chama chetu ni mkubwa sana, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inajaribu
kwa kila namna kukandamiza Upinzani na demokrasia na jambo hili si geni,
ukirudi nyuma katika historia ya vyama vya siasa nchini, hata kabla ya Uhuru,
unaweza kuona umoja ulivyoisadia TANU dhidi ya chokochoko za chama
alichoanzisha mkoloni wakati ule - United Tanganyika Party (UTP) kukabiliana na
kuidhoofisha TANU na kumzuia Mwafrika kupata Uhuru na kujitawala," alisema.
Aliwaambia vijana kwamba changamoto kama
hizo ni za kawaida kwa vyama vingi vya upinzani hasa Afrika, ambavyo vinaungwa
mkono na wananchi wengi wakiamini ni vya ukombozi.
Lakini pia alisema katika kujenga umoja
na mshikamano huo ndani ya chama, ni lazima
nguvu kubwa ipelekwe kwenye matawi waliko wananchi.
"Katika chama chochote cha siasa watu
wengi hawako ngazi za juu, bali mashinani. Ni lazima nguvu yetu kubwa ielekezwe
huko kwa sasa, ili kuhakikisha chama kinakuwa na misingi madhubuti ambayo
inaweza kutumika kukisaidia nyakati za uchaguzi," alisema.
Aidha, Lowassa ambaye katika uchaguzi
mkuu wa mwaka jana alipata asilimia 38 ya kura, alihoji umuhimu wa Serikali
kununua ndege zaidi, kuliko kupeleka huduma muhimu vijijini.
"Tumesikia nia njema yao ya kuagiza
ndege nyingine zaidi miaka miwili ijayo, lakini tunajiuliza, je isingekuwa
busara kutumia fedha hizo kupeleka maji safi na salama mijini na
vijijini?" Alihoji.
0 comments:
Post a Comment