Salha Mohamed
Advera Bulimba |
JESHI la Polisi limesema litawakamata
wazazi wa watoto watakaopotea wakati wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa
kushindwa kutekekeza majukumu yao.
Hatua hiyo imedaiwa ni kushindwa
kutekeleza majukumu yao huku watoto wakijaa katika vituo vya Polisi kutokana na
kupotea.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, alisema Jeshi hilo halitawavumilia
wazazi wa watoto watakaopotea nyakati hizi za sikukuu.
“Utakuta watoto wanajaa kwenye vituo vya
Polisi kwamba wamepotea…sasa tunajiuliza amepotea mzazi wake alikuwa wapi? Lazima
mzazi awajibike na tutamchukua mzazi aweze kuisaidia Polisi kutwambia kwa nini
mtoto wake amefika kituo cha Polisi yeye alikuwa wapi,” alisema.
Bulimba ambaye pia ni Kamishna Msaidizi
wa Jeshi hilo, alisema katika sikukuu hizi wazazi wanakuwa na tabia ya kuacha
watoto wao na kwamba wanakwenda kwenye starehe kama fukweni na kutembea wenyewe
jambo ambalo hawatakubaliana nalo.
Alisema wazazi hao wataisaidia Polisi kufanya
uchunguzi kwani kupotea kwa watoto ni uzembe.
Bulimba aliwataka wananchi kuwa makini
katika kipindi hiki, kwani kuna matapeli wanaotumia majina ya viongozi kutaka
taarifa zao au fedha kutoa taarifa Polisi.
“Hatutawavumilia wanakunywa pombe na
kuendesha magari tutawachukulia hatua za kisheria, wamiliki wa kumbi za starehe
wazingatie uhalali wa leseni zao katika uingizaji watu,” alisema.
Bulimba aliongeza kuwa ni vema wamiliki
wa maduka na hoteli kufunga vifaa vya kufuatilia taarifa za wateja wao (kamera)
ili kufuatilia nyendo zao.
Alitaka wananchi wanapoona watu tofauti
na mazingira wanamoishi watoe taarifa Polisi au kumtambua mhusika
asiyefahamika.
Alisema “wananchi wakishirikiana
tunaweza kupata taarifa za kihalifu mapema na kuudhibiti, na hata wafanyabiashara
wa maduka hufanya hivyo,” alisema.
Alitaka wananchi kuwa makini na hata
kutoa taarifa za askari wazembe wanaochelewesha kutoa huduma kwa wananchi kwani
zipo taratibu za kuwawajibisha kwani wasiofanya kazi kwa weledi.
“Kuna vituo vinahamishika hivyo ni
kuhakikisha kwamba mwananchi anapata huduma haraka na kwa wepesi kama kuna
taarifa zozote waseme,” alisema.
0 comments:
Post a Comment