Mwandishi Wetu
James Mbatia |
AFYA ya Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James
Mbatia inaendelea vyema licha ya kuelezwa atachukua muda kiasi kurejea katika
hali yake ya kawaida.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo, Novemba
14 mwaka huu alifanyiwa operesheni ya mguu iliyochukua saa nne katika Hospitali
ya Zydus Ahmedabad Gujarat nchini India, alirejea nchini takribani wiki moja
iliyopita na kuendelea kuuguza kujiuguza.
Mwenyekiti huyo aliondoka nchini Novemba
10 mwaka huu, baada ya kufika India alilazwa ikiwa ni baada ya kusumbuliwa kwa
muda mrefu na maumivu ya mguu licha ya kupatiwa matibabu katika maeneo
mbalimbali bila mafanikio.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju
aliliambia gazeti hili jana kwamba: “Mwenyekiti
Mbatia anaendelea vyema kwa kweli, unajua operesheni aliyofanyiwa sio ndogo hivyo
anaendelea kujiuguza.”
Juju aliyeko mkoani Mara katika shughuli
za chama alisema licha ya operehseni hiyo, mwenyekiti mwenza huyo wa Ukawa anaendelea vyema na kuwataka wananchi kumwombea
arejee mapema katika shughuli zake za kulijenga Taifa na NCCR -Mageuzi.
Habari zaidi zilizolifikia gazeti hili
zilieleza kuwa operesheni hiyo ya mguu ni kubwa hivyo kiongozi huyo anahitaji
muda zaidi wa kupumzika na kufanya mazoezi ili kurejea katika hali yake ya
kawaida.
Mbatia aliteuliwa na Rais mstaafu Jakaya
Kikwete mwaka 2012 kuwa mbunge kabla ya mwaka jana kujitosa katika kuwania
ubunge Jimbo la Vunjo katika Uchaguzi mkuu na kuibuka mshindi, akimwacha kwa
mbali mshindani wake, Agustino Mrema.
0 comments:
Post a Comment