Fidelis Butahe
Dk. John Magufuli |
MWENYEKITI wa CCM, Rais John Magufuli,
jana alitumia dakika 42 kueleza ‘amri’ zake 10 ambazo atashughulika nazo
kuhakikisha kuwa chama hicho kinasonga mbele, ikiwamo ya kupunguza wingi wa wajumbe
wa vikao vya juu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho Ikulu, Dar es Salaam, alisema wanachama
wa CCM wanapaswa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi.
Rais aliyeanza kuzungumza saa 4.41 hadi 5.23
asubuhi mbele ya wajumbe 355 kati ya 380, pia alitaka fedha za chama hicho
kutumika zaidi katika maeneo yenye wanachama wengi, huku akipinga uwepo wa vyeo
ambavyo havijatamkwa na Katiba ya chama hicho.
Mkutano huo uliotanguliwa na wa Kamati
Kuu (CC) uliofanyika Jumapili, ulikuwa na ajenda mbalimbali, kuu zikiwa ni
kujadili tathmini ya Uchaguzi Mkuu uliopita, sambamba na kujaza nafasi za
uongozi zilizo wazi baada ya wajumbe wake kuteuliwa kuwa mabalozi.
Dk Magufuli ambaye alikiri wazi kuwa
baadhi ya mambo hayo aliyatamka Julai baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti
Dodoma, alisema, “nataka kuifanya CCM kuwa imara kwa wanachama wa chini na
kutumia fedha nyingi kwa viongozi wa chini badala ya kutumika kwa viongozi wa
juu.
“Fedha zinatakiwa kutumika kuimarisha
palipo na wanachama wengi, yaani kwa mabalozi na katika matawi…nitafurahi
nikiwa na wajumbe wachache wa vikao vya juu.”
Huku akiwa makini, Dk Magufuli alikitaka
chama hicho kuzingatia kanuni zake za uchaguzi ikiwa ni pamoja na mwanachama
kuwa na nafasi moja tu ya uongozi kuliko ilivyo sasa.
“Nataka CCM kuwa chama ambacho viongozi
na wanachama wake watasimamia kwa vitendo Katiba. Mfano vyeo ambavyo
havijatamkwa kwenye Katiba ya CCM visiruhusiwe,” alisema.
“Kama mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM,
makamanda wa umoja wa vijana, wenyeviti washauri wa UWT, walezi…najua makamanda
mtashituka kidogo lakini huo ndio ukweli.”
Pia alitaka kanuni za jumuiya za chama
hicho ziendane na matakwa ya Katiba ya CCM.
“Ningependa tuwe na chama kinachoongozwa
na wanachama badala ya mwanachama anayeongoza chama na kukifanya chama kumfuata
mwanachama badala ya mwanachama kufuata chama. Chama lazima kiendelee kuwa mali
ya wanachama,” alisema Rais Magufuli ambaye alirudia mara mbili jambo hilo.
Akisisitiza akuhusu kuimarisha CCM na
jumuiya zake, alisema, “tunataka kuwa na chama imara chenye uwezo wa kusimamia
serikali na kutetea wanyonge.
“Hatutaki kuwa na chama legelege cha
watu walalamikaji maana sisi ndio tumepewa ridhaa na wananchi kuongoza.
Viongozi wa chama ndio mtatoa maelekezo kwa viongozi wa serikali popote
walipo.”
Alisema jambo lingine ni kuongeza idadi
ya wanachama, hasa vijana huku akihadharisha uwepo wa wanachama hewa ambao mara
nyingi huibuka wakati wa kuwania uongozi.
“Kuondoa rushwa. Chama chetu ni miongoni
mwa taasisi zinazotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa na hii si siri. Rushwa
hujidhihirisha zaidi nyakati za uchaguzi ni lazima tutafute ufumbuzi wa ugonjwa
huu sugu,” alisema
Alibainisha kuwa hivi sasa hakutakuwa na
msamaha kwa watoa na wapokea rushwa ili kuhakikisha CCM inakuwa na viongozi na
wanachama waadilifu.
Pia alisisitiza suala la CCM kujitegemea
kiuchumi, kwamba ni aibu kwa chama hicho kutegemea fedha za ruzuku na watu
binafsi kujiendesha wakati kina rasilimali, viwanja na vitega uchumi vingi.
“Hatunufaiki na rasilimali zetu kutokana
na usimamizi mbovu, ubadhirifu na kuingia mikataba isiyo na tija,” alisema.
Alisema jambo lingine atakalosimamia ni kukomesha
usaliti na kuvunja makundi, kwa maelezo kuwa wapo wanachama wachache
waliokisaliti chama hicho wakati wa uchaguzi sambamba na kuendeleza makundi.
“Tunataka kuikomesha tabia hii ambayo
inakidhoofisha sana chama chetu. Nazipongeza kamati za siasa za wilaya na mikoa
ambazo zimechukua hatua dhidi ya watu waliotusaliti kwenye uchaguzi wa mwaka
jana,” alisema.
Amri 10
1.
Kupunguza wajumbe wa vikao vya
juu
2.
Kuwa na nafasi moja ya uongozi
3.
Kuondoa vyeo ambavyo havipo
kikatiba
4.
Fedha za chama kutumika kwa
viongozi wa chini
5.
Kanuni za jumuiya kuendana na
katiba ya chama
6.
Chama kuongozwa na wanachama
7.
Kuongeza idadi ya wanachama
8.
Kupambana na rushwa ndani ya
chama
9.
CCM kujitegemea kiuchumi
10.
Kukomesha usaliti na kumaliza
makundi
0 comments:
Post a Comment