Abraham Ntambara
Mohammed Mpinga |
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini
limesema litachukua hatua kali kwa kuweka mahabusu madereva watakaokiuka sheria
za usalama barabarani katika kipindi hiki cha sikukuu badala ya kulipa faini
kama ilivyozoeleka.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Kamanda wa
Polisi wa Kikosi hicho, Mohammed Mpinga, alipozungumza na vyombo vya habari akisema
kutoza faini kumekuwa hakuwafanyi madereva kuacha kuvunja sheria.
“Kitendo cha kutoza faini, kimekuwa kikiwafanya madereva
kuvunja sheria kwa makusudi, wakijua wakikamatwa watalipa faini na kuachwa,” alisema
Mpinga.
Mpinga alisema katika kipindi hiki, watu wengi hupenda
kusafiri kwenda maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza matumizi ya vyombo vya moto
barabarani ambapo pia huambatana na starehe nyingi ikiwa ni pamoja na ulevi kwa
madereva.
Alieleza kutokana na hali hiyo ya starehe na ulevi,
madereva wengi hupoteza umakini na kushindwa kuzingatia sheria za usalama
barabarani na hatimaye kusababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu wengi.
Alifafanua, kwamba kipindi hiki madereva huwa na haraka na
huendesha kwa mwendo kasi, hunywa pombe, hupenda kupita magari ambayo ya mbele
yao bila hadhari na hufanya makosa ya kizembe yanayohatarisha maisha.
Kamanda Mpinga alisema kwa kutambua hilo, wamejipanga ili
kuwatia mbaroni madereva hao na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema katika kipindi cha kuelekea mwishoni na
mwanzoni mwa mwaka mpya, wamekuwa wakifanya operesheni katika barabara zote, stendi
za mabasi ili kukagua ubora wa mabasi, mikanda, kupima ulevi madereva,
uzidishaji abiria na nauli.
Alisema katika operesheni hii inayoendelea mikoani kwa
kipindi kifupi madereva wa mabasi ya abiria wamekamatwa kwa mwendo kasi wa
zaidi ya kilometa 90 kwa saa, ambapo katika mikoa tofauti jumla ya madereva 277
walifikishwa mahakamani wakitokea mahabusu na kulipa faini ya kati ya Sh.
300,000 na Sh 600,000
Wakati huo huo, Kamanda Mpinga amekipiga marufuku Chama
cha Kutetea Abiria nchini (Chakua) kuingilia majukumu ya Kikosi cha Usalama
Barabarani na badala yake wajikite katika majukumu yao ya kutoa elimu kwa
abiria.
Alisema Chakua wamekuwa wakishirikiana nao na Mabalozi wa
Usalama Barabarani (RSA) kutoa elimu kwa abiria lakini utendaji wao umekuwa
mbaya kiasi cha kukiuka maadili na kujikita katika usimamizi wa sheria badala ya
utoaji elimu.
Aidha, alikipiga marufuku chama hicho kufanya kazi zake
mikoani hasa kwenye vituo vikuu vya mabasi na badala yake wabaki kwenye kituo
kikuu cha mabasi Ubungo (UBT) tu.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chakua, Hassan Mchangama alisema
madai ya Kamanda Mpinga hayanja ukweli na kwamba wao wamekuwa wakitoa elimu
huku hatua nyingine kwa madereva wakiwaachia polisi.
0 comments:
Post a Comment