Waandishi Wetu, Arusha
William Lukuvi |
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi, ameshuhudia Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti
akizomewa na waandishi wa habari baada ya kugoma kuzungumzia hatima ya mwandishi
wa kituo cha ITV, Halfan Lihundi aliyewekwa mahabusu kwa amri yake.
Waandishi wa habari jana walikusanyika kwenye
ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha kusubiri kuzungumza na Waziri huyo kuhusu hatima
ya Lihundi na alipotoka kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa akifuatana
na Mkuu huyo wa Wilaya, walimtaka Mkuu wa Wilaya azungumze lakini aligoma na
kukimbilia kwenye gari lake ndipo wakamzomea.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema uandishi
wa habari ni taaluma na ina Waziri husika, hivyo asingeweza kuzungumzia sakata
la kukamatwa kwa Lihundi na badala yake watafutwe viongozi wahusika wa tasnia
ya habari.
Akiwa anazomewa na wanahabari hao,
Mnyeti alisikika akilalamikia waandishi kumfuata kwani alishatoa maagizo ya
kuachwa kwa Lihundi.
"Ole wake mtu anifuate, hata hivyo
nimeshasema wamwache kwa nini wananifuata hadi huku?” Alisikika Mkuu huyo akihoji
huku akielekea kwenye gari lake akirusha mikono.
Jana asubuhi kabla ya kwenda ofisi za
Mkuu wa Mkoa kuonana na Lukuvi, waandishi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu waliazimia
kutoripoti habari za Waziri Lukuvi ambaye anatembelea wilaya ya Arumeru na
endapo atatokea mwandishi akakiuka makubaliano hayo atatengwa.
Polisi
Jana waandishi walikusanyika nje ya kituo cha Polisi cha Usa
River wakati Lihundi akiendelea kushikiliwa kwenye mahabusu ya kituo hicho cha wilaya.
Akifuatana na wakili wake, Edward
Silayo, Lihundi alitolewa nje kwa mazungumzo lakini Mkuu wa Upelelezi wa
Wilaya, alimchukua na kuamuru arudishwe mahabusu kwa alichodai kuwa kukamatwa
kwake ni amri ya Mkuu wa Wilaya.
Wakili Silayo aliposema yeye ana uhalali
wa kuzungumza na mteja wake, alijibiwa kuwa hakuna kesi iliyofunguliwa kituoni
hapo na kilichofanyika ni Lihundi kuwekwa mahabusu kwa amri ya Mkuu wa Wilaya
ambaye kisheria anaruhusiwa kumshikilia mtu yoyote kwa saa 48.
Hata hivyo, ilipofika saa 7 mchana mmoja
wa wapelelezi wa Polisi alimtaka wakili Silayo aingie kwenye chumba cha
mahojiano ili Lihundi ahojiwe na kuachwa.
Wakati mahojiano hayo yakiendelea, Mkuu
wa Upelelezi wa Wilaya ya Arumeru, alifika na kumtaka ofisa wa Polisi aliyekuwa
akimhoji Lihundi kuacha mahojiano na kuingia na Lihundi na Wakili Silayo kwenye
chumba kingine.
Wakiwa kwenye chumba hicho, Lihundi
alihojiwa upya chini ya Silayo na walipomaliza, aliachwa kwa dhamana.
Wadau mbalimbali wa habari nchini walikosoa
kukamatwa kwa mwandishi huyo kwa tuhuma za kuandika habari za kichochezi.
Ilidaiwa jana na wadau hao kuwa hatua
hiyo ilichukuliwa na Mkuu wa Wilaya kutokana na uoga wa kutojua namna bora ya kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.
Mmoja wa wadau hao ni mwandishi mkongwe
wa habari, Joseph Sabinus aliyesema kuwa kiongozi mchapakazi na mwelewa wa
majukumu yake hawezi kuogopa kukosolewa na kutaka kupongezwa tu.
“Kupongezwa ni dalili za kufungwa macho,
hivyo ni bora ukosolewe ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo,” alisema.
Alishauri viongozi wasiogope kukosolewa,
kwani jukumu la mwandishi wa habari na chombo cha habari, ni kufichua na kuibua
kero za wananchi na si kusifu viongozi.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Neville Meena alisema mwandishi wa habari ana wajibu wa kuandika kero za
wananchi na kuzungumza na Mwenyekiti wa
Kijii, Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa.
Alisema viongozi hao wanaweza
kufanikisha habari hiyo kuwa sahihi kwa kuzungumza na mamlaka husika kuhusu
kero zinazokabili wananchi katika eneo husika.
“Hatuwezi kuvumilia vitendo vya
unyanyasaji waandishi ukiendelea, lazima hatua zichukuliwe kwa kuzingatia
taaluma na kilichoripotiwa kilikuwa ni kwa faida ya nani,” alisema.
Mkurugenzi wa Habari-MAELEZO, Dk Hassan
Abbas alisema Serikali inafuatilia kupata uhakika wa tukio hilo na baadaye
kulitolea ufafanuzi.
“Bado tunaendelea kufuatilia ili kupata
maelezo kamili baada ya tukio hilo,” alisema.
Juzi Lihundi alikamatwa na polisi wa Usa
River kwa tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa za uchochezi.
Lihundi alikamatwa saa nane mchana na
askari aliyepewa agizo na Mnyeti kwa madai ya kuandika habari ya uchochezi
kuhusu malalamiko ya wananchi wanaokabiliwa na tatizo la maji.
Gwandu alilaani kitendo hicho na kusema
hatua hiyo haikubaliki kwani haikufuata taratibu.
MCT
Sijawa Omary kutoka Mtwara anaripoti
kuwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa tamko la kulaani na kutoridhishwa
na kitendo cha kukamatwa kwa Lihundi.
Tamko hilo lilitolewa jana mkoani humo
na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alipozumgumza na waandishi wa habari wa mkoa
huo aliko kwa majukumu ya kikazi.
Habari iliyoripotiwa ilihusu mgogoro wa
maji katika kijiji cha Leguruki juu ya wananchi wa kijiji hicho kukosa maji kwa
siku kadhaa.
Mukajanga alisema mwandishi wa habari ana
haki ya kupata habari na kuitoa kwa maslahi ya umma bila kuvunja sheria ikiwa
ni moja au sehemu ya majukumu yake.
“Suala la kumfanya mwandishi wa habari
ashindwe kutimiza majukumu yake kikatiba ni kinyima uhuru wa vyombo vya habari
pia ni kumfanya mwananchi ashindwe kupata habari kama haki yake ya msingi na
kikatiba,” alisema Mukajanga.
Alisema Serikali inataka utendaji wa
uwajibikaji, kufichua na kupambana na vitendo viovu ikiwamo rushwa lakini inashangaza
kuona mwandishi akitekeleza sehemu ya majukumu yake anakuwa mchochezi hivyo
kumnyima uhuru wa kufanya kazi yake kikamilifu.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa
Mtwara (MTPC), Hassan Simba alisema wanahabari wa mkoa wanalaani kitendo cha kukamatwa kwa mwandishi huyo,
kwani ni udhalilishaji dhidi ya waandishi wa habari nchini na duniani kote.
Imeandikwa na Seif
Mangwangi (Arusha), Sijawa Omary (Mtwara), Leonce Zimbandu na Sharifa Marira
(Dar es Salaam).
0 comments:
Post a Comment