*Ni mmoja kati ya 85 waliookeketwa, kufichwa majumbani
Dotto Mwaibale
MTOTO mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni
mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivule katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es
Salaam (jina linahifadhiwa) ameelezea jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka wazazi
wake ili asikeketwe.
Mtoto huyo hivi sasa analelewa na
msamaria mwema baada kufungua kesi katika Kituo cha Polisi cha Stakishari
Ukonga kufuatia kufikishwa kituoni hapo kwa ajili ya kujisalimisha na kuelezea
madhila aliyotaka kufanyiwa.
Wakati mtoto huyo akijisalimisha katika
kituo hicho, kuna taarifa za ndani kuwa kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85
wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 15 katika manispaa hiyo ambapo watoto zaidi ya
30 wanaeleezwa kuwa tayari wamekeketwa.
Akizungumza na JAMBOLEO, mtoto huyo
alisema hawezi kurudi nyumbani kwao akihofia kupigwa na kukeketwa, badala yake
anaomba msaada wa hifadhi kutoka kwa Watanzania.
"Baada ya baba yangu kufariki
nyumbani kwetu Tarime tulikuja na mama hapa Dar esSalaam kwa kaka yake Chacha
Nyanchiri anayeishi Kitunda Kivule karibu na Shule ya Msingi Misitu"
alisema mtoto huyo.
Alisema katikati ya wiki iliyopita
alifika bibi yake mzaa baba aliyemtaja kwa jina moja la Boke na kuwaambia yeye
na wenzake wajiandaa kwenda kukeketwa.
Mtoto huyo alisema kwamba Alhamisi
majira ya saa mbili usiku wakiwa nyumbani kwa mjomba wao anakoishi na mama yake,
alifika bibi mzaa mama yake aliyemtaja kwa jina moja la Debora, huku akiwa
ameongozana na mama yake na kuwaambia yeye na watoto wengine wawili wa mama
yake mkubwa wakaoge ili waende kukeketwa.
Alisema ili kukwepa kukeketwa
alipokwenda bafuni alifanikiwa kutoka na kupita njia nyingine na kufanikiwa
kuwatoroka wazazi wake na kwenda kujificha kwenye pagala na ilipofika saa tatu
usiku, alifika eneo la kwa Mpemba akielekea darajani ambako alikutana na dada
mmoja aliyemsimulia mkasa huo.
Alisema dada huyo alimchukua hadi
nyumbani kwake ambako alilala na siku iliyofuata alimpeleka kituo cha Polisi
cha Stakishari kwa ajili ya usalama wake.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye
alikataa kutaja jina lake alisema kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85 kabla ya
kuisha kwa mwaka huu wa 2016 na kuwa karibu watoto 30 wamekwishakeketwa.
Alisema shughuli hiyo inasimamiwa na
wazee wa kimila wa kabila la Kikurya na kuwa ngariba mkuu wa kazi hiyo ya
kukeketa watoto hao yupo eneo la Nyamuhanga na kuwa baada ya kukeketwa hufanyiwa
sherehe kwa siri katika baadhi ya nyumba zilizopo jirani na ngariba huyo.
Mwenyekiti wa Serikali wa mtaa anaoishi
mtoto huyo, Dominick Mlimi alisema hana taarifa ya mtoto huyo kutoweka nyumbani
kwao.
"Jana niliwaona baadhi ya watoto wa
kike wa familia ya Nyanchiri wakiwa hapo barabarani, lakini kuhusu kutoweka kwa
mtoto huyo kwa kuhofia kukeketwa sijazipata" alisema Mlimi.
Mke wa Chacha Nyanchiri ambaye anaishi
na mtoto huyo Regina Wilson alikiri mtoto huyo kuondoka usiku baada ya kufika
nyumbani hapo bibi yake na mama yake ingawa alisema hawakutoa taarifa kwa mtu
yeyote ya kutoweka kwake.
"Mwenye mamlaka ya mtoto huyo ni
mama yake ambaye ametoka asubuhi kwenda kumtafuta mtaani, mimi sihusiki naye na
wala sijui walichomwambia, ingawa siku zote tulipokuwa tukizungumzia kuhusu
kukeketwa mtoto huyo alikuwa akionesha hofu," alisema Wilson.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala,
Salum Hamdun alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo ingawa aliahidi
kuwasiliana na wasaidizi wake ili kulifuatilia na baadaye kutoa taarifa kamili.
Mtoto huyo alisema watoto wenzake
waliofanyiwa vitendo hivyo bado wapo majumbani mwao wakijiuguza majeraha na
kama vyombo vya usalama vitahitaji kwenda kuwaonyesha walipo yupo tayari.
Taarifa ambazo tumezipata jana kutoka
kwa baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na nyumba aliyokuwa akiishi mtoto huyo
na mama yake, zimeeleza kuwa polisi walifika katika nyumba hiyo na kumkamata
Regina Wilson, mama wa mtoto huyo Happyness na watu wengine wawili na kupelekwa
kituo cha polisi Stakishari kwa mahojiano.
0 comments:
Post a Comment