*Yasemekana si rahisi kaburi Lake Kuonekana
*Mtaalamu ashauri itumike damu yake iliyopo
Fidelis Butahe
WAKATI wahifadhi wanyamapori wakieleza kuwa
mkakati wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kumsaka faru John kwa kuchukua vinasaba
hautafanikiwa kwa sababu hakuna kaburi lake, wataalamu wa wanyamapori na
vinasaba wamesema kaburi si njia pekee ya kujua ukweli kuhusu kifo cha mnyama
huyo.
Baadhi ya vyombo vya habari jana vilinukuu
baadhi ya wahifadhi wakieleza kuwa hakuna kaburi la faru huyo, kwa kuwa
hakuzikwa na kwa maana hiyo mpango wa kupima vinasaba utakwama.
Lakini, jana wataalamu hao waliieleza
JAMBO LEO, kwamba kitu chochote kutoka kwa kiumbehai kinaweza kuchukuliwa na
kupimwa vinasaba, huku wakisisitiza kuwa haiwezekani mnyama mkubwa kama faru
afe miezi miwili tu kisha kusiwe na mabaki yanayoweza kuchukuliwa kama sampuli.
Ufafanuzi huo wa kitaalamu ulitolewa zikiwa
zimepita siku tatu tangu Serikali ieleze kuundwa timu ya kuchunguza utaratibu
wa kuhamishwa kwa faru huyo aliyeripotiwa kufa Agosti 18, kutoka Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro (NCAA) kwenda hifadhi ya Faru Weusi ya Sasakwa iliyoko Grumeti.
Katika maelezo yake, Waziri Majaliwa
alitaka kufukuliwa kwa kaburi la faru huyo anayeripotiwa kufa, kuchukua vinasaba
vya masalia yake na kisha kwenda NCAA kuchukua vinasaba vya watoto wake na
kuvilinganisha na pembe alizopelekewa kama ushahidi wa kifo hicho.
Majaliwa alitoa kauli hiyo licha ya
Desemba 9 kupokea taarifa ya kuhamishwa kwa faru huyo, huku Waziri wa Maliasili
na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akisema alihamishwa kwa sababu ya kupunguza
tatizo la kuzaliana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Sakata hilo liliibuka Desemba 6 baada ya
Waziri Mkuu Majaliwa akiwa ziarani Arusha, kuuagiza uongozi wa NCAA, kumletea
nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru huyo kutoka kwenye hifadhi hiyo,
ndani ya siku mbili.
Licha ya kuletewa taarifa hizo na
kuelezwa kuwa mnyama huyo amekufa, Majaliwa alihoji aliumwa lini, daktari gani
aliyemtibu na zilipo taarifa za matibabu yake na kuagiza mwili wa faru huyo ufukuliwe
na kutazama kama vinasaba vyake vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wako kwenye
bonde la Ngorongoro.
Mmoja wa madaktari wa wanyamapori ambaye
aliomba kutotajwa jina gazetini ili kutoathiri uchunguzi wa tukio hilo, alisema:
“Yule ni mnyama wa porini, si binadamu. Akifa kinachoondolewa ni nyara za Serikali,
si kubebwa na kuzikwa mahali, ila pale alipofia watu huamini ni kaburi.
“Huwezi kusema vinasaba vyake havipo, vinapatikana
sehemu nyingi sana, kuna ngozi zinabaki pale (alipofia), mifupa. Si kwamba mnyama
akioza anaisha kila kitu hapana. Ngozi ya faru ni ngumu sana na inabaki muda
mrefu sana. Haiwezi kutoonekana kwa miezi miwili tu, hata na mifupa yake!”
Alisema kama ngozi ya tembo inaweza
kukaa miaka miwili na bado alama zake zikabaki, haiwezekani ngozi ya faru
ikatoweka kabisa tena ndani ya miezi miwili tu, “inaweza kukaa takribani mwaka
mmoja.
“Bado kuna mabaki yake, hata umbile lake
unaweza kuliona na kujua huyu faru amefia hapa, yule ni mnyama mkubwa si
sungura, kwamba unaweza kumla na kutafuna mifupa yote,” alisema daktari huyo
aliyeeleza anafanya shughuli zake kwenye mbuga mbalimbali nchini kwa hiyo
anajua mambo mengi.
Daktari huyo alibainisha kuwa hata
katika kumhamisha mnyama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ni lazima
achukuliwe damu, huku akihoji kuwa kama hata hiyo damu nayo haiwezi kupatikana.
“Mnyama yule amekufa, vinasaba vyake haviwezekani
vikakosekana. Nafikiri Serikali inafanya vizuri, kila mtu awe macho, kwamba usifanye
kitu ukajificha kichakani, wafanye uchunguzi ili kubaini ukweli. Hakuna mtu kufanya
ujanja ujanja kama zamani,” alisisitiza.
Wakati mtaalamu huyo akieleza hayo, Dk
Absalom Maiseri wa hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam, alieleza jinsi ya
kuchukua vinasaba kwamba, “wanachukua sampuli ya vitu vyote iwe manyoya, mate
au mbegu za uzazi.
“Vinasaba viko ndani ya kina cha seli.
Vinasaba ndio vimebeba chembe za urithi zenye maelekezo ya shughuli za mwili
ikiwamo mwonekano wote.
Alisema pembe za faru John zinaweza
kuchukuliwa sampuli na kulinganishwa na sampuli yoyote kutoka kwa watoto 26 wa
mnyama huyo.
“Wahandisi wa vinasaba watachambua
vinasaba vya pande zote mbili na kulinganisha kitaalamu, ikiwemo kutazama kama
malighafi za chembe za urithi ndiyo hizo zilizopo kwa uzao wake (watoto wake),”
alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment