Sharifa Marira
Asiatu Msuya |
NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Asiatu Msuya, amesema taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba ofisi
hiyo imepiga marufuku watumishi wake kupewa mikopo na taasisi za fedha nchini
mpaka ithibitike kuwa hawadaiwi mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HESLB), si za kweli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
ofisi hiyo jana, haina mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu mtumishi kukopa kwenye
taasisi yoyote ya fedha.
"Ikumbukwe kuwa mikopo yote ya
watumishi wa umma kwenye taasisi za fedha, hutolewa kwa kuzingatia sharia,
kanuni na taratibu zilizopo, ilimradi mtumishi awe na vigezo,” alisema Msuya.
Aliwataka watumishi wa umma
kutojihusisha na usambazaji taarifa za uongo na kuzingatia maadili ya utumishi
wa umma.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi
na Utawala Bora, Angella Kairuki alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu uwepo wa
taarifa hizo, alisema: ‘’Hilo ni agizo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
lililotolewa kwa wafanyakazi wake, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kazi.’’
Alipoulizwa kama ni tamko linalopaswa
kutekelezwa kwa watumishi wote wa umma, alisema Ofisi ya AG ndiyo yenye jukumu
la kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tangazo limetoka ofisi yake.
‘’Unazungumzia tangazo lililo kwenye
mitandao ya kijamii, ni kweli nimeliona, lakini limetolewa na Ofisi ya AG
ambaye leo (jana) alikuwa anazungumza na
waandishi wa habari kuhusu suala hilo hilo, sasa nadhani ingekuwa vizuri
mkawasiliana naye, sipaswi kuwazungumzia,’’ alisema Kairuki.
Taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ilielekezwa
kwa wakurugenzi wa divisheni, wakuu wa vitengo, mawakili wa serikali wafawidhi,
mikoa na wilaya na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Barua hiyo ambayo ilisainiwa na mtu
anayeitwa Kabungo ilihusu utaratibu wa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.
“Mnaombwwa kuwataarifu watumishi walioko
chini yenu, kuwa kuanzia sasa mtumishi atakayehitaji mkopo kwenye taasisi za
fedha pamoja na mahitaji mengine ya taasisi hizo, ili kupata mkopo, atatakiwa
pia kuwasilisha uthibitisho wa kama hana mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu, maombi ambayo hayataambatana na uthibitisho,
hayatashughulikiwa,” iliosema barua hiyo.
0 comments:
Post a Comment