Peter Akaro
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu jana
alitumia hadhara ya Ibada ya Krismasi kuwapoza waathirika wa tetemeko la ardhi
lililoukumba mkoa huo hivi karibuni, akisema misaada yote inayotolewa inasimamiwa
na Serikali.
Akizungumza katika Ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika kitaifa
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini
Magharibi Bukoba, Kijuu mbali na kuwapongeza waliotoa misaada hiyo, alisema
hakuna msaada utakaotumika kinyume kwa kuwa inasimamiwa na kamati ya maafa ya
mkoa ambayo yeye ndiye mwenyekiti.
“Serikali inaendelea kutoa shukrani kwa mashirika, taasisi, kampuni
na wahisani wote kwa namna walivyoguswa na kujitokeza kuchangia,” alisema
Kijuu.
Alisema tetemeko hilo lililoua watu 17 na kuacha majeruhi 440,
lilisababisha uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu na kuacha simamzi kubwa
mioyoni mwa watu wengi.
“Nawashukuru viongozi wetu wa dini zote kwa jinsi walivyoshirikiana
na serikali kwa kuwafariji waadhirika waliopatwa na maafa haya,” alisema Kijuu.
Katika hatua nyingine aliwashukuru viongozi wote wa dini mkoani Kagera
na madhehebu yote kwa ushirikiano pamoja na serikali kwa kuhakikisha wanatekeleza
majukumu yao kikamilifu na kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja.
“Mmeweza kudumisha amani, upendo, utulivu pamoja na kuvumiliana
pale linapotokea jambo ambalo linataka kutugawanya katika Imani zetu,” alisema
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT)
Moses Matonya, alisema Jumuiya hiyo imeitika wito wa Serikali wa kuwasaidia kwa
hali na mali watu walioathirika na tetemeko hilo.
“CCT kupitia shirika lake imetoa mchango na kuuwasilisha kwa Mkoa
wa Mkoa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment